Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Wednesday, August 21, 2013

Nchimbi atosa kumpa ulinzi Dk Mwakyembe

NCHIMBI
 WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi
 
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi amepiga chenga kuzungumzia suala la kumpa ulinzi Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Hoja ya Dk. Mwakyembe kutakiwa kupewa ulinzi limepigiwa kelele na watu wengi, wakiwemo viongozi wa dini ambao walidai kuwa kazi anayofanya ya kupambana na dawa za kulevya ni nzito.
Kwa sababu hiyo, waliomba Mwakyembe awekewe ulinzi ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri ya kukabiliana na wauzaji na wasafirishaji wa dawa hizo kwani ni hatari kwa nchi na watu wake.   Hatua hiyo imekuja baada ya Dk. Mwakyembe kuagiza maofisa kadhaa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wafukuzwe kazi kwa kile alichodai walishiriki kusaidia wasafirishaji wa dawa hizo katika uwanja huo.   Kutokana na hali hiyo, waandishi wa habari jana walikuwa na kiu ya kusikia kama Dk. Nchimbi atatangaza kumpa ulinzi Mwakyembe ili aweze kufanyakazi hiyo vizuri zaidi.   “Ninajua wengi mnataka kuniuliza maswali (la Mwakyembe), nje ya mada yangu, hivyo sipo tayari kuyajibu leo, labda nitayaweka kiporo.
“Mimi nilikuwa mwandishi wa habari kama nyie, hivyo nikitoka nje kidogo ya mada yangu ninayotaka kuizungumzia leo, nikijibu tu maswali yenu najua kabisa mtakwepesha suala langu la uhamiaji ambalo ndilo ninalozungumzia hapa leo hii,” alisema Dk. Nchimbi.
Mwenyekiti wa Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Sheikh Alhad Salum alisema juzi kuwa taifa linateketea kutokana na watu wengi kuathirika na dawa hizo.
Kuhusu Dk. Mwakyembe na harakati zake za kupambana na dawa za kulevya katika uwanja huo, Sheikh Salum alisema baraza linampongeza kwa uzalendo, ujasiri, upendo na huruma yake kwa taifa.   “Dk. Mwakyembe ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wote nchini, baraza linawaomba viongozi wa dini wa imani zote tumuombee, uthubutu huu ni hatari kama tusipompa ushirikiano.
“Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere tusikubali kuwa njia ya kuu ya kupitisha dawa haramu za kulevya.
“Ndiyo maana tunaweka wazi kuwa Dk. Mwakyembe ameonesha dhamira ya kupambana na dawa hizo. Pia ni jukumu letu ni kumpa ushirikiano maana akiachwa pekee yake hatafanikiwa,” alisema.
Sheikh Salum alisema kwa mtazamo wao wanaona ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kumpa ulinzi wa kutosha ili afanyekazi yake vizuri.
“Tunapaswa kushirikiana katika vita hii maana ni kubwa. Hata hivyo, kutaja majina ya wanaojihusisha na biashara hii ni jambo linalotaka uthubutu wa hali ya juu.
“Tena tunasikia kuwa mtandao wa dawa za kulevya unahusisha hata baadhi ya vigogo serikalini na hata viongozi wa dini. Tunapaswa kupambana kwa nguvu zote ili tushinde vita hii ngumu,” alisisitiza.

Source: Jambo Leo

No comments:

Post a Comment