Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Thursday, August 15, 2013

Mbowe: Katiba Mpya inahitaji hekima, busara

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema, kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kupata Katiba Mpya siyo kazi rahisi, ni kazi inayohitaji nia ya dhati ya taifa zima, kwa kuwa katiba ni mali ya wananchi na rasilimali za taifa.
Mbowe alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara wa kukujadili Rasimu ya Maoni ya Katiba, uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo wilayani Musoma Mkoa wa Mara hivi karibuni.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa kazi hiyo, Chadema wameamua kuzunguka nchi nzima kwa lengo la kutoa elimu ya Katiba kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kutoa ufafanuzi wa maana ya Katiba na kujibu hoja za wananchi hao.
Alisema kuwa Tanzania ambayo ilikuwa ikisifika kama nchi ya amani na mshikamano kwa miaka mingi, sasa inaelekea kubomoka na hali hiyo inatokana na katiba mbovu isiyokuwa na mipaka ya madaraka ambayo sasa tumeamua kuifanyia mabadiliko.
“Hebu angalieni sasa hivi kuna ugomvi wa dini, wananchi na Serikali hususan katika maeneo yaliyo na madini, vyombo vya usalama na raia na mengine mengi. Je hii ndiyo Tanzania yenye amani na mshikamano aliyoiacha Hayati Baba wa Taifa?” alihoji Mbowe.
Alisema katika kuzungumzia Katiba hakuna vyama vya siasa, polisi wala mtu wa kada nyingine yoyote. Katiba ni mali ya Watanzania wote, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutoa maoni yake juu ya mambo anayoamini kuwa yatalisaidia taifa kama yataingizwa kwenye katiba.
Awali akihutubia katika mkutano huo,Mmbunge wa Ubungo John Mnyika, alisema kuwa maadili ya uongozi na utawala bora, vinatikiswa kama siyo kuyumbishwa. Aliwataka wananchi kuhakikisha misingi ya taifa inarekebika kupitia marekebisho ya katiba mpya.
Mnyika alisema kuwa katika kupitisha maoni ya katiba, wanataka haki, uwazi na usawa katika masuala ya madini na rasilimali za nchi ambazo kimsingi zinapaswa kutajwa kwenye katiba. Tunataka Katiba pia impunguzie rais madaraka, alisema.
Alisema gharama za maisha ya wananchi zinazidi kupanda kila kukicha kutokana na rais kuwa na mlimbikano wa madaraka, hivyo kufanya maamuzi bila kutambua kuwa wananchi walio na kima cha chini ndio wanaoumia.
Aidha alisema kuwa anashangazwa na serikali ya CCM inavyokataa mfumo wa serikali tatu kwa madai kuwa,serikali tatu ni gharama kubwa sana kuendesha huku wakisahau baraza kubwa la mawaziri lisilo na meno.
Chadema imekuwa ikifanya mikutano ya hadharani nchini kuzungumzia mchakato wa katiba. Wamekuwa wakitoa elimu na kuwaeleza wananchi umuhimu wa kazi hiyo kwa taifa.

No comments:

Post a Comment