Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Wednesday, August 14, 2013

Muungano wazua mjadala Mwanza


Wajumbe wa Baraza la Katiba wilayani Nyamagana, wamechafua hali ya hewa na kumweka mwenyekiti wa baraza hilo, Muhamed Mshamba katika wakati mgumu baada ya kuibuka makundi mawili yaliyokuwa yakivutana kuhusu Muundo wa Muungano.
Wakati kundi moja likiwa linatetea Muundo wa Serikali mbili, lingine likataka Serikali tatu. Kundi linalotaka Serikali tatu limeeleza kuwa Serikali mbili kufanya kazi ilizotumwa za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Akichangia hoja hiyo, mwakilishi wa wananchi wa Kapripot, Milton Rutabana alisema kuwa, Muungano wa Serikali mbili umeshindwa kutatua kero nyingi,  ikiwemo fursa za maendeleo katika nyanja za uchumi, siasa na jamii.
Alisema kuwa Serikali mbili za Muungano zimekiuka makubalianao yaliyowekwa kwenye hati ya Muungano ya mwaka 1964. “Ilitakiwa kuwa na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika, Jamhuri ya watu wa Zanzibar kwa jina la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema.
Aliendelea kufafanua na kudai kuwa mambo ya Muungano yalikuwa mawili tu mwaka huo wa 1964, lakini sasa hivi yameongezeka na kufikia mambo 22 bila ya ridhaa ya wananchi kutoka pande zote mbili za Muungano.
Hoja hiyo ya Rutabana ilizua  vurugu katika kikao hicho baada ya upande wa pili kuona kuwa wanazidiwa hoja katika kutetea Serikali mbili na kudai kuwa ili waweze kukubali Serikali tatu, Tume ihakikishe inapata hati halisi ya makubaliano ya Muungano ili waweze kufanya uamuzi.
Rutabana aliendelea kueleza kuwa Serikali za Muungano kwa jina la Tanzania imeinyima utambulisho nchi ya Zanziabar na hivyo kuifanya isiweze katika vikao vya kimataifa ikiwamo vya UN, OIC, Fifa na E.A.C.
“Ni muhimu sasa kuwepo na Serikali tatu ili tupate sehemu ya kupeleka malalamiko yetu ya kimaendeleo kama Serikali ya Zanzibar ilivyo na Rais wake, bendera yake na wimbo wake wa Taifa,” alisema Rutabana na kuongeza;
Mjumbe wa baraza hilo kutoka Igoma Adamu Chagulani, alidai kuwa Serikali mbili za Muungano zimekuwa kikwazo kikubwa cha kutatua kero za Muungano, ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu huku wabunge wa Zanzibar wamekuwa wakitunga sheria au kukataa sheria kwa mambo ambayo ni ya Muungano.
Alisema kuwa kuna haja ya kurejea matakwa ya kuwa na Serikali tatu kama historia ndefu inavyojionyesha hali iliyopelekea baadhi ya watu kujazwa chuki baada ya kudai Serikali tatu.
Alisema kuwa kuanzia kwa utawala wa Abdu Jumbe mwaka 1984 Zanzibar kulichafuka sababu hiyo ya Serikali tatu, mwaka 1990, G55 wabunge walidai kuwe na Serikali tatu na madai hayo yalikuwa chini ya Waziri mkuu Malecela na baba wa Taifa alifanikiwa kuzimisha.
“Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 ilitaka Serikali tatu, Tume ya Jaji Kisanga 1998 ilitaka Serikali tatu, Tume ya Jaji Warioba 2012 nayo imekuja na majibu hayo hayo,” alisema Changulani.

No comments:

Post a Comment