UVCCM imemtaka Rais wa Zanzibar Dr Shein kumfukuza kazi Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud Othman kutokana na kauli yake kuwa suluhisho la kero za muungano ni serikali tatu tu na sio vinginevyo, msimamo ambao ni kinyume na CCM wanaotaka serikali mbili tu. Mwanasheria mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Othman Masoud aliuponda mfumo wa serikali mbili kuwa ni ghali na inawagharimu zaidi Wazanzibar .

Naibu katibu Mkuu wa UVCCM (Z'bar) ndie aliyetoa kauli hiyo ya kumtaka Dr Shein amchukulie hatua Mwanasheria huyo Mkuu wa SMZ wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari makao makuu ya UVCCM Z'bar eneo la Gymkhana.

Huu ni mwendelezo wa sintofahamu ndani ya CCM wenyewe kwa wenyewe katika sakata la Katiba Mpya. Ikumbukwe aliyekuwa waziri wa SMZ Mansoor Himid juzi amefukuzwa uanachama wa CCM kutokana na kuwa na misimamo inayokinzana na ile ya chama chake cha CCM ambapo yeye alikuwa (na bado) anapigania Zanzibar kupewa hadhi kamili ya utaifa kwa kuwepo na muungano wa mkataba.