Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Saturday, August 17, 2013

Katiba ni uhai wa taifa - Dk. Slaa

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amewaasa Watanzania kutambua kuwa Katiba ni uhai wa taifa, hivyo wawe huru kutoa maoni ili baadaye iwatetee na kuwalinda.
Dk. Slaa alisema hayo katika mkutano wa kukusanya maoni ya Katiba mpya uliofanyika katika viwanja vya Tangamano jijini hapa juzi.
Katika mkutano huo maelfu ya wananchi walikusanyika kutoa maoni ya Katiba mpya.
Alisema chama chake kimeamua kukusanya maoni kwani Katiba si mali ya chama, bali ni ya Watanzania wenyewe hivyo wameona ni vema kuwakusanya kwa pamoja kutoa maoni yao ambayo ni haki ya kila Mtanzania.
Dk. Slaa alisema wenye mawazo ya kufanana wana uwezo wa kutengeneza Katiba itakayowalinda na wala si itakayolinda chama chochote cha siasa.
Alisema Katiba iliyopo inatumiwa vibaya na viongozi walioko madarakani kwa sababu wale wanaouvunja maadili kwa kuiba rasilimali za umma hawachuliwi hatua.
Akizungumza zaidi katika mkutano huo alisema serikali tatu itapunguza gharama za uendeshaji kwa kuokoa fedha nyingi kwani asilimia ya wabunge na mawaziri itapungua kwa kiasi kikubwa.
Pia aliwata Watanzania kuacha woga katika kudai haki kwani kufanya hivyo ni kutojitendea haki, hata Mungu anakataza.
Naye mjumbe wa Kamati Kuu wa CHADEMA, Mabere Marando, alisema watahakikisha wanawafikia Watanzania na kuwaelewesha Rasimu ya Katiba Mpya na msimamo wa chama hicho.
Hata hivyo alisema chama hicho kitawafikia wananchi katika maeneo yao kuwaelewesha na kupata maoni, hivyo ni vema kusema nini wanataka kiwemo katika Katiba hiyo mpya.

No comments:

Post a Comment