Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Thursday, August 15, 2013

CHADEMA: Hatuhitaji utashi wa mtu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesisitiza kuwa sheria ya mabadiliko ya Katiba mpya ndiyo inavyowaruhusu kukusanya maoni wala si utashi wa mtu.
Akizungumza jijini Arusha juzi katika kikao cha baraza la kitaasisi la kukusanya maoni ya kuboresha rasimu ya Katiba mpya yanayoratibiwa na chama hicho, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mabere Marando, alisema wako sahihi.
“Kifungu cha 18 (1) (2) cha sheria ya mabadiliko ya Katiba ndicho kinaagiza hivyo wala si utashi wa mtu,” alisema Marando katika viwanja Kilombero kwenye mkutano aliohutubia pia na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.
Alisema kuwa kifungu hicho cha sheria ya marekebisho ya Katiba mpya, kinavitambua vyama vya siasa kama taasisi na hivyo kuweza kutoa mapendekezo ya maoni ya rasimu ya Katiba sawa na mabaraza ya wilaya.
“Wananchi endeleeni kutoa maoni yenu nawahakikishia Jaji Warioba apende asipende ni lazima ayapokee mapendekezo haya,” alisema.
Marando alitaja mambo manne makuu wanayoyataka yaingie kwenye Katiba kuwa ni suala la Tume Huru ya Uchaguzi ambapo Rais anyang’anywe mamlaka ya kuteua mwenyekiti wa tume hiyo na wajumbe wake.
“Tunaunga mkono mapendekezo ya rasimu ya Katiba ya kutaka wajumbe hao waombe nafasi hizo, wadahiliwe na kuthibitishwa na Bunge kisha majina yapelekwe kwa Rais ambaye atayatakangaza bila kufanya marekebisho yoyote,” alisisitiza.
Marando alisema kuwa wanapendekeza uwepo uwazi kwenye uendeshaji wa serikali hasa kwenye masuala ya mikataba ambayo kwa muda mrefu imefanywa siri na hivyo kupora rasilimali za taifa.
Naye Dk. Slaa aliitaka CCM kuacha unafiki wa kudai kwamba serikali tatu itaongeza gharama za uendeshaji, na kusisitiza kuwa kama wanataka kupunguza gharama wangependekeza serikali moja.
Alitoa mfano akisema kuwa muundo wa sasa wa serikali mbili idadi ya wabunge wote pamoja na wawakilishi ni 438 wakati kwa muundo wa serikali tatu idadi itapungua na kubaki 314.
Dk. Slaa alisema kuwa ni vema Rais na watumishi wote wa umma waondolewe kinga ya kutoshtakiwa pindi wakiwa na wakitoka madarakani ili kuongeza uwajibikaji.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, ameendelea kuzitaka taasisi mbalimblai kuacha kuwashawishi maoni wafuasi wao katika mchakato wa kujadili rasimu.
Akizungumza mjini Dodoma jana baada ya ufunguzi wa utoaji wa maoni katika mabaraza kwa watu wenye ulemavu, alisema kuwa kuna matatizo makubwa ambayo yanaonekana kujitokeza nchi nzima kwa taasisi mbalimbali kuwatumia wananchi kutoa maoni kwa maslahi yao.
“Wajumbe wameanza kuingiliwa na taasisisi mbalimbali pamoja na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa badala ya kuwaacha kutoa maoni yao,” alisema.
Kuhusu suala la serikali tatu, alisema kuwa Watanzania wasiwe na wasiwasi kwa kudhani kuwa itakuwa na gharama kubwa.

No comments:

Post a Comment