Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Monday, August 19, 2013

Madiwani Bukoba: Tuko tayari kwenda Chadema

 Na Arodia Peter 

MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliofukuzwa katika Manispaa ya Bukoba, wamesema wako tayari kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kama chama chao kitaendelea na msimamo wa kuwafukuza. Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, mmoja wa madiwani hao (jina na kata yake tumevihifadhi), alisema wako tayari kuhamia Chadema muda wowote kama hawatarudishiwa uanachama wao.

Alisema, madiwani wote waliofukuzwa wana msimamo mmoja, ambapo wanasubiri vikao vya Kamati Kuu ya CC ili wajue hatima yao, lakini vikishindwa kuwarudisha kwenye chama, watahamia Chadema ili kuendeleza harakati zao walizozianzisha.

Alisema, wanachokifanya wao ni kutetea maslahi ya taifa na wananchi waliowapigia kura na si kulinda biashara za watu binafsi, hata kama wanaungwa mkono na uongozi wa juu wa CCM.

Msimamo huo wa madiwani umekuja siku mbili baada ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kuwakaribisha madiwani hao katika chama chake na kusema wako tayari kuwafundisha siasa za mageuzi.

Mbowe aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru, mjini Bukoba, juzi, katika mwendelezo wa mikutano ya mabaraza ya wazi ya chama hicho kujadili rasmu ya Katiba mpya.

Mbowe alikwenda mbali zaidi akisema chama chake kiko tayari kushirikiana na kiongozi wa CCM anayepinga ufisadi kama anavyofanya Mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki.

Alipoulizwa kama wamepata mawazo ya kujiunga na Chadema, baada ya kauli ya Mbowe, diwani huyo alisema wao walikwishakuwa na mawazo hayo, lakini kauli ya mwenyekiti huyo imewaweka huru zaidi.

“Si kama tumeamua sasa, mawazo ya kuhamia Chadema tulikuwa nayo baada ya uongozi wa mkoa kutangaza kutuvua uanachama, lakini kwa kauli ya Mbowe kutukaribisha rasmi, kumetujengea ari mpya kwamba hatujapotea.

“Tatizo letu na meya linafahamika kwamba ni ufisadi wake tulioulalamikia tangu mwaka jana, kwenye vikao vya Baraza la Madiwani, hatukusikilizwa, badala yake tunaonekana wasaliti wa chama.

“CCM wanapaswa kujua kwamba, hoja za wapinzani zikiwa sahihi wananchi wanawaunga mkono, vivyo hivyo na sisi hatuwezi kubeza hoja zao kwa sababu tu ni wapinzani, tutaonekana watu wa ajabu,” alisema diwani huyo.

“Tumefarijika na kauli ya Mbowe, baadhi yetu tulikuwepo katika mkutano wake jana (juzi) pale Uwanja wa Uhuru, ni suala la muda tu mtasikia Bukoba imezaliwa upya,” alisema.

Mbali na hilo, mgogoro huo unaofukuta katika Halmashauri ya Bukoba unahusishwa na sababu za kisiasa kati ya Kagasheki na Meya wa mji huo, Anatory Amani.

Balozi Kagasheki, ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), anatajwa kuwa na uhasama wa kisiasa na kada mwenzake, Amani, ambaye awali wawili hao walikuwa na ushirika wa karibu.

Madiwani wanane waliofukuzwa wanatuhumiwa kushirikiana na wenzao wa upinzani kusaini hati maalum na kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kumng’oa madarakani Meya Amani mwishoni mwa mwaka.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kilichokaa Agosti 3, mwaka huu, kiliwafukuza uanachama na uongozi madiwani hao, akiwamo Mwenyekiti wake wa Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na Diwani wa Kata ya Kashai.

Wengine waliofukuzwa mbali na mwenyekiti huyo, ni Diwani wa Kata ya Buhembe, Alexander Ngalinda, ambaye pia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.
Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment