Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Thursday, August 15, 2013

COSOTA acheni kukwamisha stika za TRA

 Khadija Kalili     

KARIBU mpendwa msomaji wa safu ya Busati, bila shaka mu wazima wa afya na mnaendelea na majukumu ya ujenzi wa taifa.
Au baada ya salaam, leo nitazungumzia mada ya stempu ana stika za kuweka katika albamu za wasanii na jinsi Chama cha Hatimiliki Tanzania (Cosota), wanavyolalamikiwa kuwa na urasimu.
 
Nikiwa katika pitapita zangu za mitaani, yaani vijiwe mbalimbali ambako huwa natafuta la kuandika, nikasikia baadhi ya watu wakilalamika urasimu wa barua ya utambulisho kutoka Cosota, ili waweze kupata stika za kubandika kwenye albamu zao na kuuza.
“Yaani haiwezekani hadi leo Cosota wanashindwa kutupatia barua ya kututambua ili tuweze kupata stempu za kutuwezesha kusambaza albamu zetu,” chanzo hicho kilisikika kikilalama.
Ni hivi, kwa ufupi serikali imerasimisha kazi za wasanii na hakuna yeyote itakayeingia sokoni bila ya kuwa na stika ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), sasa na kama ni kweli Cosota bado wana banabana, hii haijakaa sawa, kwani wezi nao wapo watatumia akili zao zingine ili kuendelea kuiba kazi ya msanii ama wasanii.
Huu urasimu uliopo Cosota wa kushindwa kuwapa ruksa kwa maandishi au barua ya utambuzi wasanii, ili waweze kuendelea kufanya mambo yao kwa kisingizio cha kusimamia mirahaba kwanza, hakina mashiko kabisa.
Nasema hakina uzito, kwa sababu kama msanii, bendi au kundi, fulani wametoa albamu zao huku wakiwa wametumia gharama kubwa, kama tunavyojua kuwa kuingia studio ni fedha, kurekodi video ni fedha, sasa hizo fedha zitarudi vipi huku ikiwa albamu haiko sokoni?
Cosota mnapaswa kwenda na wakati na kubadilika katika namna ya kufanya kazi; wimbo au albamu inapoingia sokoni, ndipo kila mdau huwa anapata kiu ya kuikimbilia, lakini kwa kukalia kutoa uamuzi wa kuwaonyesha njia wasanii ya kusonga mbele ili biashara iendelee, hapo mtaua muziki.
Katika hili, siyo kuua tu muziki, bali ni kwamba mtaua familia za watu wengi kwa sababu zenu binafsi ambazo hazina mashiko. Nauliza hivi hiyo mirahaba italipwa vipi ilhali mnachangia kuchelewesha albamu kuingia sokoni?
Inachosha kuona kwamba labda mnataka kila wakati mtupiwe lawama licha ya kwamba yule aliyekuwa akiwakera wasanii, Yustus Mkinga, ameondolewa kwani bado mambo ni yaleyale, wasanii wanalalamika, haipendezi.
Binafsi, nakumbuka nikiwa katika uwajibikaji wa kazi, nilifika ofisi za Cosota huku nikihitaji kupewa msaada wa kikazi, lakini jambo la kushangaza, nilianza kupewa mlolongo wa utaratibu ambao usingenisaidia zaidi ya kunicheleweshea kile kidogo nilichokuwa nakitafuta kutoka kwao.
Nilijaribu kutoa ushawishi wangu na kujieleza, lakini haikusaidia, jambo ambalo likanifanya nitoke na maswali mengi, hivi kama mambo ndiyo hivi, hakuna sababu ya chombo kama hicho kuwepo, tena kikishindwa kutoa ushirikiano katika masuala nyeti ya habari, ambayo kila kunapokucha, lazima habari mbalimbali ziwepo duniani.
Katika malalamiko ya urasimu wa Cosota, nathubutu kusema na wao wanachangia katika uvujishaji wa miziki ya wasanii, kwani kama kuna albamu, halafu hakuna utambuzi wowote Cosota wa barua ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ina faida gani?
Hapa naweza kusema, kwa mfano mpita njia kila siku anapita nje ya duka ambalo halina mlango wala mlinzi yeyote, huku akiangalia ndani anaona kuna bidhaa za kumvutia, ipo siku ataamua kunyakua na kwenda zake, haijalishi atauza kwa bei ya hasara kiasi gani, kwake ni faida kwa kuwa hajatolea jasho kile anachokiuza.
Vivyo hivyo, madhara ya kuchelewesha upatikanaji wa stempu kwa wasanii ambao kazi zao ziko tayari, kutasababisha watu kuiba hata CD moja, halafu kuzisambaza kwa njia wanazozijua wao, hii itakuwa ni hasara kwa mwenye mali, iwe ni msanii mmojammoja, bendi au kikundi.
Ushauri kwenu ni kwamba msikae ofisini mkasubiri wasanii wawafuate, basi na ninyi kwa kuwa mnalipwa mishahara na serikali na hizo ni fedha za walipa kodi ambao pia ni haohao wanamuziki, warahisishieni kwa kuwapa mapema barua ili waweze kwenda kununua stika za kubandika kwenye kazi zao wauze.
Mfano hai ambao hauna ubishi ni kwa bendi ya Twanga Pepeta, ambao walizindua albamu yao miezi miwili iliyopita, lakini wao wanathibitisha kwamba waliandika barua Cosota ya kuomba kibali waweze kwenda TRA kwa ajili ya manunuzi ya stika, lakini jambo la kushangaza hadi sasa hawajajibiwa lolote.
Sababu yao kubwa Cosota ikiwa ni ileile, wana kazi kubwa ya kugawa mirahaba kwa wasanii, kazi ambayo wameimaliza wiki iliyopita huku wakidai kwamba watashughulikia wiki hii inayomalizika leo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya The African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka, anasema kwamba yeye binafsi kwa albamu zake nne ametumia zaidi ya sh milioni 15 ambazo atazirudisha kwa mauzo, lakini hadi sasa hawajaweza kuingia sokoni.
“Cosota wana urasimu, mfano Twanga walizindua albamu yao Juni 30, lakini haiwezi kuuzwa kwa sababu hatujapata stika za TRA, utaratibu bado haujaeleweka, sisi tunahitaji barua ya kututhibitisha TRA kuwa sisi ndiyo wahusika halali wa kazi iliyorekodiwa, ili tuweze kununua stika na ni lazima wao watuthibitishe kuwa ni halali, sasa wanapotuchelewesha ni kwamba, hata kimauzo pia tutachelewa, kwani chuma hupindwa kikiwa cha moto,” anasema Asha.
Cosota ambao wako chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, hadi hapo wanaonyesha kushindwa kufanya kazi zao na sio kila kitu aambiwe waziri, huenda wameshindwa labda, lakini hivi wanashindwaje kujigawa kikazi kwa mtu mmoja akashughulikia mirabaha na mwingine usajili?
Kwa ucheleweshaji huu, Cosota ni wazembe na mnawakosesha TRA fedha nyingi ambazo wanamuziki na wasanii wangelipa kwa kununua stika.

No comments:

Post a Comment