Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Thursday, August 26, 2010

Mr II Sugu asema yeye si mwanasiasa

 Joseph Mbilinyi(Mr II - SUGU) hapo akisisitiza jambo kwa furaha

MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Joseph Mbilinyi ‘Mr II Sugu’ amesema yeye si mwanasiasa kama anavyotazamwa na baadhi ya wanajamii bali ni mwanaharakati wa masuala ya maendeleo nchini.
Hayo aliyaeleza juzi, alipokuwa akirejesha fomu ya kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Sugu alisema kuwa, harakati zake za kutetea jamii alizianza miaka 15 iliyopita kupitia tasnia ya sanaa ya uimbaji, hivyo kwa sasa anataka kuendeleza harakati hizo kupitia majukwaa ya siasa.
“Naomba nieleweke kuwa mimi si mwanasiasa, bali ukweli mimi ni mwanaharakati wa masuala ya maendeleo ya jamii na ninachokifanya sasa, ni kubadilisha jukwaa kutoka jukwaa la sanaa ya muziki na kutua katika jukwaa la siasa,’’ alisema Mbilinyi.
Aidha alipoulizwa na Tanzania Daima kuwa ni vitu gani anavyofikiri ni kipaumbele cha wananchi wa Jimbo hilo la Mbeya Mjini linaloongozwa na Benson Mpesya, alikana kueleza kwa undani, kwa kile alichodai kuwa wakati wa kampeni ukifika, ndipo atakuwa na fursa ya kuyadadavua yale yote ambayo wananchi wamemweleza kutaka kusaidiana naye.
Mbilinyi alidokeza kuwa kitu kinachomkera zaidi ni siasa za makundi ambazo zinaendelea kulizorotesha kimaendeleo jimbo hilo, ambalo kihistoria ni lenye neema lakini ni jimbo pekee duniani ambalo halina barabara licha ya kuitwa jiji.
“Nakerwa sana na siasa za makundi zinazoendelezwa na baadhi ya viongozi waliopo madarakani, lakini niwe wazi kuwa, nimewahi kuimba wimbo unaohusu Mbeya na maisha ya watu wake, lakini ukweli ni kwamba nina mapenzi mema na Mbeya zaidi ya kuuimbia nyimbo,’’ alisema Sugu.
Awali Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija, alisema kuwa, kuchukua fomu kwa Mbilinyi siyo tiketi ya kumsimika kupeperusha bendera ya chama hicho, bali hatima ya kumpata atakayepeperusha bendera ya chama hicho itakuwa Julai 24 mwaka huu, ambako hadi sasa wengine waliojitokeza kuomba ridhaa hiyo ni Gwakisa Mwakasendo, Eddo Makata na Daudi Mponzi.

No comments:

Post a Comment