Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Thursday, August 26, 2010

(Habari zilizopita) Mr II kuibeba Chadema Ubunge Mbeya Mjini


Pichani katika ni Mwanamuziki muasisi wa Bongo fleva nchini Mr 2 (Sugu) akionyesha kitambulisho kwa kutambulika rasmi kuwa mwanachama wa chama cha Chadema.Kushoto kwake ni Bw John Mnyika wa Chadema aliyemkabidhi Mr 2 Kitambulisho hicho.

Brandy Nelson

MSANII mkongwe wa  muziki wa kizazi kipya, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Mr II, ameteuliwa kuiwakilisha Chadema kugombea ubunge wa jimbo la Mbeya Mjini baada ya kushinda kwenye kura za maoni.

Mbilinyi alichaguliwa jana kwednye mkutano wa kura za maoni zilizopigwa na wanachama wa chama hicho jijini  Mbeya.

Akitangaza matokeo ya kura hizo, msimamizi wa kura za maoni wa Chadema, Sambwee Shitambala alisema mgombea huyo ameshinda baada ya kupata kuwa kura 175 ambazo ni sawa na asilimia 48.3 ya kura 362 zilizopigwa.

 Shitambala, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema mkoani Mbeya, alisema Mbilinyi alimshinda mpinzani wake kwa tofauti ya kura 53. Mpinzani huyo, Daud Mponzi alipata kura 122.

Mgombea mwingine ambaye ni mwandishi wa habari, Christopher Nyenyembe alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 54 na Gwakisa Mwakasendo aliambulia kura tisa.

Mapema, Shitambala aliwataka wajumbe wa mkutano huo kumchagua mtu mwenye sifa, anayekubalika na anayeuzika kwa kuzingatia hali ya kisiasa katika Jimbo la Mbeya Mjini  ili Chadema iweze kuibuka na ushindi.

Shitambala  ambaye pia ni mgombea wa kiti cha ubunge katika Jimbo la Mbeya Vijijini, alisema katibu mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Peter Slaa amempigia simu na kumtaka awaeleze wanachama hao kuchagua mtu makini.

Kabla ya uchaguzi, mwanachama mmoja alimtaka Mbilinyi aeleze namna atakavyofanya ili kukiwezesha chama hicho kuwa na ofisi nzuri kuanzia ngazi ya kata.

Akijibu swali hilo, Mr ll alisema ubunge wake utakuwa shirikishi kwa wanachama wote na kuwa atajitahidi kutafuta wafadhili wa kusaidia ujenzi wa ofisi hizo.

Sugu amekuwa mtetezi mkubwa wa haki za wasanii nchini akipinga ukandamizaji unaofanywa na baadhi ya wamiliki wa vituo vya redio nchini, mameneja na makampuni.

Sugu alikuwa mmoja wa wasanii wa kwanza wa muziki wa rap ya Kitanzania kujizolea mashabiki wengi, kiasi cha kufuatwa na lundo la watu kila alipoonekana hadharani.

Lakini baada ya kukorofishana na baadhi ya makamapuni ya muziki alianza kutoweka kutokana na nyimbo zake kutopewa nafasi kwenye vipindi vya redio na televisheni.

No comments:

Post a Comment