Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Sunday, September 5, 2010

Maaskofu wasusia mwaliko wa JK

*Ni kushirikiana naye kula futari
Mwandishi Maalum, Mbeya

MAASKOFU wa makanisa ya Kikristo na wachungaji mkoani Mbeya walioalikwa kula futari (kufuturu) na Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ndogo alipokuwa katika ziara za kampeni hivi karibuni, walikataa kwa maelezo kuwa hawawezi kushiriki naye kwa kuwa ni mgombea wa urais.
Habari ilizozipata Mwananchi Jumapili zinaeleza kuwa maaskofu na wachungaji hao walimgomea Rais Kikwete Septemba Mosi, mwaka huu wakati wa ziara yake mkoani Mbeya.
Gazeti hili lilifanya juhudi kumtafuta Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba kutoa ufafanuzi wa taaarifa hizo jana.
Hata hivyo alipopatikana kuzungumzia suala hilo Makamba alisema kwa kifupi, "hilo mimi sijui, silijui hilo".
Kwa mujibu wa mwaliko huo ambao Mwananchi Jumapili iliuona, viongozi hao walitakiwa kufika Ikulu ndogo saa 12 jioni mjini Mbeya kufuturu pamoja na Rais Kikwete.
Baada ya kupokea mwaliko huo, viongozi hao wa dini walisema kufuturu na Rais Kikwete wakati huu wa kampeni kungeweza kuvunja uaminifu wao kwa waumini kwa vile Kikwete ni sawa na wagombea wengine wa urais wanaostahili kupatiwa haki sawa.
Habari hizo zimedai kuwa mbali ya maaskofu na wachungaji wa dini mbalimbali takribani 40 walioalikwa kula futari hiyo, mwaliko huo pia uliwahusu viongozi wa dini nyingine.
Viongozi hao wa dini walisema mwaliko huo haukuwa na manufaa yoyote kwa viongozi wa kikiristo ambao hawakufunga hivyo wasingeweza kushiriki futari inayopaswa kuliwa na ndugu zao Waislamu waliofunga.
Hii ni mara ya kwanza katika uchaguzi huu viongozi wa dini kutakaa mwaliko wa rais Kikwete.
"Sisi maaskofu mkoani Mbeya ambao tulialikwa juzi (Jumanne) kwenye futari Ikulu ya Mbeya tumetafakari pamoja na wenzetu ambao hawakualikwa kuwa kitendo hiki ni rushwa ya chakula".
"Tunakilaani vikali kitendo hiki tumejiuliza kwa nini tualikwe kwa futuru sisi ambao hatuko kwenye mfungo? Tena tumechukizwa sana na mgombea, kufanyiwa zindiko uwanjani na machifu wakati amefunga," ilieleza sehemu ya waraka wa maaskofu hao kwa Mwananchi Jumapili.
Akiwa katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya wazee wa kimila (machifu) wa Usafwa mkoani humo walimvisha Kikwete mgolole, kumpa kiti cha kichifu pamoja na mkuki kama ishara ya kumkubali na kuahidi kuwa wananchi wote wa Mbeya watampigia kura Kikwete.
Mmoja wa Maaskofu aliyepata nafasi ya kuzungumza na Mwananchi Jumapili alisema wameugomea mwaliko huo na kuufananisha na rushwa akieleza kuwa wao hawakupaswa kualikwa kipindi hiki ambacho jamii nzima ya watanzania inawatazama viongozi wa dini na kutaka kujua wameegemea upande upi.
Askofu huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kuwa si msemaji wa umoja wao, alisema ni vyema viongozi wa madhehebu ya dini wakawa makini katika kipindi hiki cha kampeni.
Kwa mujibu wa mwaliko huo uliowataka waalikwa wote kuwa nadhifu waalikwa hao walitakiwa kufikisha jibu kwa mpambe wa rais Ikulu iwapo watahudhuria au la.
Askofu wa Kanisa la Pentekoste Evangelisti, Zebadia Mwanyerere Mwakatage alipohojiwa alisema kuwa hakupata mwaliko huo, lakini akasema kwamba hata angeupata asingekwenda kwa kuwa kitendo cha kualikwa na rais akiwa mgombea hakikustahili.
Mwakatage alisema ni makosa viongozi wa dini kushiriki kwenye mialiko ya wagombea uongozi na kwamba, Kikwete anatumia kofia yake akijua kuwa yeye ni mgombea sawa na wengine hali ambayo askofu huyo alisema ingempa shida iwapo angehudhuria.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wakristo Mkoa wa Mbeya, Askofu John Mwela wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini alisema anaungana na msimamo wa maaskofu wenzake na wachungaji waliokataa kuitikia mwaliko huo kwa kuwa kwa kufanya hivyo wangekuwa wanapingana na msimamo walionao wa kutompendelea mgombea yoyote.
Askofu Mwela alisema alipatiwa kadi ya mwaliko iliyochelewa kumfikia na kwamba hata angeipata mapema asingeweza kwenda kwa kuwa hakufunga Ramadhani na kwamba, kuhudhuria hafla hiyo ingempa shida kwa waumini wake kwa vile hatakiwi kushabikia upande wowote wa siasa.
“Naunga mkono maamuzi ya wenzangu waliokataa kwenda Ikulu, kama waliliona hilo ni vyema tukawa na msimamo, tatizo huyu ni mgombea sawa na wengine na isitoshe ingekuwa tumealikwa kwenye dhifa hapo tungeenda kula chakula sio kufuturu hatukufunga sasa ningeenda kufanya nini huko,” alisisitiza Askofu Mwela.
Kiongozi huyo wa madhehebu ya kikiristo Mkoa wa Mbeya aliwataka waumini wa madhehebu hayo kuwa makini kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu na kuwahimiza kuhudhuria kwenye mikutano ya vyama vyote kuwasikiliza wagombea ili kuchagua viongozi bora.
Askofu wa Kanisa Katoliki, Evaristo Chengula alipotafutwa kutoa maoni yake kuhusu mwaliko huo wa Ikulu ilidaiwa kuwa amesafiri nje ya mkoa huo sambamba na maaskofu wengine Alinikisa Cheyo wa kanisa la Moraviani na Thomas Daminius Kongoro wa Pentekoste Assembless Of God(PAG) wote hawakuweza kupatikana kutoa maoni yao au kuthibitisha kama walikuwa miongoni mwa waalikwa.
Umoja wa makanisa ya kikiristo unaunganisha madhehemu manne ya Jumuiya ya Kikiristo Tanzania(CCT), Makanisa ya Kikatoliki (TEC), Jumuiya ya Kipentekoste (PCT) na makanisa huru ambayo, Mwenyekiti wake ni Askofu Mwela wa Anglikani.

No comments:

Post a Comment