Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Friday, September 17, 2010

Joseph Mbilinyi ataka bandari ya nchikavu Mbeya

MGOMBEA ubunge wa jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi amewaahidi wananchi wa Mbeya kuwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge atahakikisha serikali inaweka bandari ya nchi kavu mkoani hapa ili kuwarahisishia kazi wafanyabiashara wa nje na kukuza maisha ya wakazi wa mjini hapa.

Mbilinyi, mmoja wa wasanii waliotangaza muziki wa kizazi kipya akitumia jina la Mr ll 'Sugu' alitoa kauli hiyo wakati wa kampeni zake akisema wakati umefika wakati kwa mkoa wa Mbeya kuwa na bandari ya Nchi kavu ili kuwezesha wafanyabiashara wanaotoka nchi jirani za Zambia na Malawi kupata bidhaa kirahisi mkoani hapa badala ya kusafiri hadi Dar es salaam.

Mbilinyi alisema Mbeya imekosa mkakati wa kusaidia wafanyabiashara kutoka nje kupata bidhaa zao mkoani hapa na ndio maana hupitiliza kwenda Dar es salaam kufuata bidhaa, wakati mji huu ni kiungo kikubwa cha kibiashara na nchi za Malawi na Zambia.

Alisema mfumo wa biashara mkoani hapa umekua kikwazo kwa wafanyabiashara wengi ndio maana hata wafanya biashara wa Mbeya wamekimbilia Dar es salaam kuendeleza biashara na kuutelekeza mkoa wao.

“Tukiwa na ushirikianao mzuri baina ya serikali na wafanyabiashara na kuwa na bandari ya nchikavu itasaidia wafanyabiashara kutoka Malawi, Congo, Zambia na Zimbabwe kununua bidhaa zao hapa na kuongeza mapato kwa serikali ya Mbeya,” alisema Mbilinyi.

Alisema watoto wa mkoani hapa wamekuwa wakichangishwa michango mingi kwenye shule zao kutokana na serikali ya mkoa kutokuwa na vyanzo vingi vya mapato.

Mbilinyi pia alisisitizia ahadi yake ya kuhakikisha kila shule ya Mbeya Mjini inakuwa na kompyuta 30 ambazo alisema zitapatikana kutoka kwa wafadhili ili kusaidia wanafunzi kielimu.

"Sijaja kuihubiri Chadema, bali nimekuja kukomboa Mkoa wa Mbeya na hasa jimbo la Mbeya Mjini ili kuweka heshima ya jiji kwa wakazi wake kuwa na maisha yenye kupendeza... ni aibu kuona mkoa wa mbeya unapendeza pembezoni huku katikati kukiwa na maisha mabovu kwa wananchi," alisema.

"Maendeleo hayahitaji wageni toka nje ya nchi bali kushirikiana kwa pamoja kutasaidia jamii yetu."

1 comment:

  1. Hongera babu, usisahau ahadi ulizotoa kwa wananchi, hasa maji, umeme, afya, elimu, huduma za jamii na miundo mbinu.

    Kila la heri.

    ReplyDelete