Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Monday, September 9, 2013

PROF. LIPUMBA, MNYIKA WAMKABA NDUGAI

na Asha Bani


VYAMA vya CHADEMA na CUF vimezidi kumwandama Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa hatua yake ya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani akiwemo kiongozi mkuu wa kambi hiyo, Freeman Mbowe.
Wakati Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akilaani kitendo hicho cha Ndugai kumzima Mbowe na kuamuru askari wamtoe nje kwa nguvu, alikiita ni cha udhalilishaji na kisichokubalika; sekretarieti ya CHADEMA imeitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kupokea taarifa ya masuala mbalimbali yaliyojitokeza bungeni na kisha kutoa uamuzi wa nini kifanyike.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Prof. Lipumba alisema kuwa kitendo hicho ni cha aibu hakikupaswa kufanywa na Naibu Spika wa Bunge kwani angesimama Waziri Mkuu Mizengo Pinda asingeweza kumnyima nafasi ya kuzungumza.
“Sisi CUF tunajiuliza, angesimama Pinda kuongea Naibu Spika angemnyima nafasi? Angethubutu kuamrisha askari wamtoe nje?
“Kwa nini haya yanatendwa kwa mpinzani na hayawezi kutokea kwa kiongozi wa serikali?” alihoji.
Lipumba pia alihoji kama serikali ina mamlaka makubwa katika Bunge kuliko Bunge lenyewe hadi kiti cha Spika kiendeshe masuala kwa taratibu za kupendelea serikali.
Alisema kwa kuwanyima haki wabunge wa upinzani hasa kiongozi wao wa pande zote mbili ni njama za wazi za serikali na kiti cha Spika kutelekeza maoni ya wananchi na kuyapatia kipaumbele yale ya CCM kwa maslahi yao.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kufanya hivyo kunaondoa uhalali wa Bunge na kiti cha Spika katika kusimamia mchakato huo huku akitaja moja ya njama za wazi kuwa ni pamoja na ile ya wabunge 166 wa Bunge la Katiba wanaopaswa kupendekezwa na taasisi mbalimbali na kuteuliwa na rais.
“CUF tumesikitishwa na mabadiliko yaliyofanywa na lengo la CCM la kupitisha muswada unaompa mamlaka ya uteuzi rais kwani hivi sasa kila taasisi bila kujali uzito wake husika itapaswa kuteua majina tisa na kumpa rais na kisha atateua jina moja au asiteue kabisa jina lolote,” alisema.
Alifafanua kuwa sheria hiyo inampa rais mamlaka kuteua watu anaowataka kuwa wajumbe wa Bunge la Kutunga Katiba.
Prof. Lipumba alisema CCM na serikali yake inajua kuwa hujuma wanazozifanya katika mchakato wa Katiba ndizo zitawapa Katiba wanayoitaka wao kama chama na haitakuwa na uhalali wa wananchi.
Alisema kuwa ombi la wabunge wa upinzani kuwa muswada huu urudishwe kwa wananchi na kwa kamati kujadiliwa upya lilikuwa na mantiki kubwa, kwamba msimamo wao kupinga muswada huu unapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania.
Lipumba pia alizungumzia kitendo cha kudhalilishwa kwa wabunge akiwemo mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kwa kupigwa waziwazi na askari ndani ya Bunge na kisha kutupwa kama mzigo nje ya lango.
Alisema pia mbunge wa viti Maalum CUF, Mozza Abeid, kuvuliwa vazi lake la hijabu ni udhalilishaji mkubwa kwa wanawake na usiokubalika.
Alisema CUF inaendelea na juhudi ya kuwasiliana na viongozi wa vyama vingine ili kuweka mkakati wa pamoja wa kukabiliana na hujuma dhidi ya mchakato wa kupata Katiba mpya.
CHADEMA wakutana
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mkurugenzi wa habari na uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kikao chao cha sekretarieti kitakuwa chini ya Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa.
Alisema kiongozi wa wabunge wa chama hicho atatoa taarifa ya yaliyojiri wakati wa kujadili muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013 ambayo itajadiliwa na wajumbe wa kikao hicho.
Mnyika alisema jambo kubwa watakaloliangalia katika kikao hicho ni tafsiri ya mambo yote yaliyotokea kabla muswada huo haujafikishwa bungeni ikiwamo uamuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuingilia kati mchakato huo kwa manufaa yake.
“Yaliyotokea Septemba 4 hadi 6 bungeni yalipangwa kwa sababu maalum na hii ni baada ya CCM kuona kila mwanya waliotaka kuutumia kukwamisha rasimu ya katiba umeshindikana sasa wakaamua walitumie Bunge,” alisema.
Mnyika alisema katiba ni ya wananchi na kwamba kitendo chochote cha kuihujumu ni mbinu ya kuwanyima kupata haki ya msingi ya kusikilizwa.
Aliongeza kuwa kwa sasa mwelekeo wa kuwa na katiba mpya itakayotumika mwaka 2015 haupo na kwamba hicho ndicho CCM inakitafuta kwa nguvu zote baada ya kuona wananchi kutaka muundo wa serikali tatu.
Alisema CHADEMA haiamini katika katiba isiyojali maslahi ya wananchi na kwamba uharaka wa kukimbilia suala hilo hauna maana kwa kuwa suala la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 linaweza kutungiwa kanuni zake huku mchakato wa kupata katiba bora ukiendelea.
“Madai ya katiba ni zaidi ya vyama vya upinzani, tutafanya taratibu ya kukutana na wadau mbali mbali nchini kwa ajili ya kutoa uamuzi wa pamoja,” alisema.
Mnyika alisema njama za kuhakikisha wabunge wa upinzani hawapati nafasi ya kujadili rasimu ya sheria ya mabadiliko ya katiba zilianza mara baada ya rasimu kutolewa hali aliyoeleza kuzua hofu kwa CCM.
Alisema hata maazimio ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyokutana na wadau mbalimbali yaliathiriwa na kikao cha CCM kilichokutana mjini Dodoma ambapo jukumu hili lilirudishwa kwa wabunge wao kwa ajili ya kuhakikisha katiba ya Watanzania haifanikiwi.
“Kamati ya wabunge wa CCM ilipewa jukumu hilo na mtekelezaji mkuu akiwa ni yule atakayekaa katika kiti cha spika kuhakikisha wabunge wa upinzani hawatoi hoja zao,” alisema.

No comments:

Post a Comment