Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Friday, May 6, 2011

CHADEMA WAMSHAMBULIA PROF. MWANDOSYA

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Mr II Sugu, amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Mark Mwandosya, kutumia muda wake wa uongozi uliosalia kwa ajili ya kujiandaa na kustaafu kwa kuwa ndoto zake za kutaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haziwezi kutimia.
Pia alisema ni vigumu tena kwake kuendelea kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki.
Sugu aliyasema hayo wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa ‘Chadema Twanga Kotekote’ ulofanyika katika kijiji cha Kandete, eneo la Mwakaleli Jimbo la Rungwe Mashariki ambalo hivi sasa linashikiliwa na Prof. Mwandosya.

Mkutano huo ni moja ya mikutano mingi itakayoendelea kufanyika katika jimbo hilo, ambayo imepewa jina la ‘Operesheni Giant Ndosya, yenye lengo la maandalizi ya kumg’oa Prof. Mwandosya katika jimbo hilo kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Sugu alisema Prof. Mwandosya hajalitendea haki jimbo lake kwa kuwa wananchi hao wamempa ridhaa ya kuwaongoza kwa zaidi ya miaka 15, tena akiwa na wadhifa mkubwa serikalini, lakini kwa muda wote huo ameshindwa kuwajengea wananchi wake barabara kuanzia Katumba hadi Mwakaleli yenye urefu wa kilometa 30 tu.
Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi Joseph Mbilinyi (SUGU) akiwa jukwaani kwenye moja ya mikutano
Alisema hata kama Prof. Mwandosya akichaguliwa kuwa rais hatawakumbuka wananchi wa Rungwe na badala yake atafanyia sherehe za kujipongeza Dar es Salaam, kwa kuwa huku kwao hakuna barabara alizojenga anazoweza kupitisha magari ya Ikulu.
Aidha Sugu alisema anamshangaa Prof. Mandosya kutotumia elimu kubwa aliyonayo kusoma alama za nyakati na kuendeleza fikra za kutaka urais akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho Sugu alidai kuwa kuna kila dalili kwamba kufikia mwaka 2015 chama hicho kinaweza kisiwepo.
“Nawaomba siku akija hapa mpeni ujumbe huu kuwa ajiandae kustaafu kwa kuwa hakuna urais wala ubunge tena kwake, namshauri arudi kufundisha darasani kwa kuwa hilo ndilo bado tunalihitaji kutoka kwake,” alisema Sugu huku akishangiliwa.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Eddo Mwamalala, alisema mikutano ya Twanga Kotekote wilayani Rungwe ambayo imeongezewa jina la ‘Operesheni Giant Ndosya’ inalenga kung’oa meno ya Mwandosya ya utawala wake wa kiimla katika Jimbo la Rungwe Mashariki.
Mwamalala alisema Mwandosya amewalemaza wakazi wa Rungwe Mashariki kimaendeleo na kuwa katika hilo hawawezi kumwonea huruma, hivyo akawataka wananchi wa Rungwe Mashariki kuunga mkono harakati hizo za ukombozi wao.
“Hakuna kumwonea huruma Mwandosya kwa kuwa ametulemaza kimaendeleo, hata hawa madiwani wabovu mliowachagua mmewachagua kwa jina la Mwandosya, kubwa tunalowaombeni wananchi wa Rungwe ni kutuunga mkono katika harakati hizi za ukombozi wa jimbo hili,” alisema Mwamalala.
Kiongozi wa kikosikazi cha Chadema Twanga Kotekote, John Mwambigija, alisema Mwandosya badala ya kufikiria maendeleo ya jimbo lake ameanza kampeni chafu ya kuwarubuni na kuwanunua viongozi wa Chadema na kuwaingiza CCM.
Alidai kuwa kwa kitendo hicho cha Mwandosya ajue kuwa jimboni kwake hayuko salama. Alisema Mwandosya asahau tena ubunge mwaka 2015 na kama anahitaji kupona akimbilie kugombea urais.
Timu hiyo ya Kikosikazi Chadema Twanga kotekote leo inahamia mjini Tukuyu katika jimbo linaloongozwa na aliyekuwa Waziri wa Afya, Prof. David Mwakyusa, kwa ajili ya kuendeleza harakati zake za kukijenga chama.
Baada ya mkutano huo, Chadema Twanga Kotekote itasitisha mikutano yake ili kupisha maandalizi ya maandamano ya kitaifa ya Operesheni Sangara ambayo yanatarajiwa kufanyika Mei 4, mwaka huu jijini Mbeya.

No comments:

Post a Comment