Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Dar es Salaam. Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imebaini mtandao wa ufisadi unaoshirikisha wakurugenzi 70 wa halmashauri mbalimbali hapa nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk alisema keshokutwa atataja majina ya wakurugenzi hao ili wananchi waweze kuwafahamu.
Mbarouk alisema kuwa Tanzania Bara ina halmashauri 134, kwa hiyo ina maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na mambo hayo.
“Baadhi ya wakurugenzi hao walihamishwa kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali, lakini bado wanajihusisha na mambo haya,” alisema Mbarouk.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imepanga kukutana kesho na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia ili kuzungumzia suala hilo.
“Kuna zaidi ya wakurugenzi 70 wako kwenye mtandao wa ufisadi kwa kushirikiana na watendaji wa Hazina na Tamisemi, jambo ambalo limesababisha halmashauri zao kupata hati chafu kwa miaka mitano mfululizo,”alisema Mbarouk.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana na wahasibu wao katika kutumia vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe ambapo halmashauri yake imefanya vibaya katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hajachukuliwa hatua na badala yake amekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Alisema mbali na halmashauri hiyo, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Rhoda Nsemwa ambaye alisimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ufisadi, lakini bado anaendelea kupata mshahara na stahiki zake kama mtumishi aliye kazini.
“Tumeshangaa kuona kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo bado anaendelea kulipwa mshahara, kodi ya nyumba na marupurupu mengine kama ofisa aliye kazini wakati ana kesi ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali,” alisema.
Alibainisha kamati hiyo pia imebaini kuwa Takukuru inajihusisha moja kwa moja na vitendo vya rushwa, kutokana na kupotosha ukweli wa taarifa za watuhumiwa na kuchelewesha kuwasilisha jalada mahakamani.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment