MAANDAMANO ya amani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza ya kupinga uchaguzi batili uliomweka madarakani meya wa manispaa hiyo, Henry Matata, jana yalihitimishwa kwa mabomu ya machozi kutoka jeshi la polisi.
Mbali na meya pia CHADEMA wanampinga naibu wake, Swila Dede, pamoja na hatua ya kufukuzwa kienyeji madiwani wao watatu kinyume cha taratibu na sheria za nchi.
Madiwani wanaodaiwa kufukuzwa na meya Matata kinyume cha sheria na kata zao kwenye mabano ni Abubakar Kapera (Nyamanoro), Malietha Chenyenge (Ilemela) na Dany Kahungu wa kata ya Kirumba wote wa CHADEMA.
Maandamano hayo ya amani yaliyokuwa na baraka za jeshi la polisi, yaliyoanzia eneo la Buzuruga saa 5 asubuhi hadi viwanja vya Furahisha, lakini dosari ilikuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, kushindwa kufika uwanjani hapo kuyapokea kama ilivyotarajiwa.
Ilielezwa kuwa katika vikao vya mazungumzo baina ya viongozi wa CHADEMA na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, Ndikilo aliridhia kuyapokea maandamano hayo na kwamba badala yake hakuonekana uwanjani hapo.
Kufuatia hali hiyo, ujumbe wa viongozi wa CHADEMA ukiongozwa na mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, na madiwani watatu wanaodaiwa kufukuzwa na Matata kinyume cha sheria ulienda ofisini kwa mkuu wa mkoa kuzungumza naye kama alivyoagiza afuatwe na watu wachache ofisini kwake wakazungumze.
Katika mazungumzo hayo yaliyokuwa ya vuta nikuvute baina ya mkuu wa mkoa na viongozi hao wa CHADEMA yaliyodumu takribani dakika 45 hivi na kushindwa kupata mwafaka wake, wafuasi wa chama hicho walidai kuchoka kusubiri majibu ya serikali.
Baada ya wafuasi hao kuchoka kusubiri, waliamua kuanzisha maandamano upya kutoka viwanja vya Furahisha kuelekea ofisi ya mkuu wa mkoa, lakini askari polisi walizuia hali hiyo maeneo ya makutano ya barabara ya Makongoro na Mwaloni Kirumba.
Kufuatia hali hiyo, polisi wa FFU waliokuwa na silaha za kivita na mabomu ya kutoa machozi, walilazimika kupambana na maelfu ya wananchi hao, huku raia wakirusha mawe na polisi nao wakirusha mabomu.
Ghasia hizo zilizodumu zaidi ya saa moja, huku polisi hao waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa wa Mwanza, Joseph Konyo, wakifanikiwa kuwadhibiti wafuasi hao kwa kuwatawanya ingawa nguvu kubwa ilitumika huku milio ya risasi ikisikika katika viunga vya jiji.
RC na CHADEMA
Katika kikao hicho ndani ya ofisi ya mkuu huyo kabla hali haijachafuka, mbunge Kiwia aliwasilisha madai mawili makuu.
Moja likiwa la kupinga uchaguzi wa meya na naibu wake katika manispaa ya Ilemela na pili kupinga kufukuzwa kinyemela madiwani wao watatu.
Alisema kuwa manispaa ya Ilemela inao madiwani 14 na kwamba Novemba 9, 2012, ulifanyika uchaguzi wa meya na madiwani sita pekee ndio waliopiga kura bila kukidhi akidi ya theluthi mbili ya wajumbe.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa, tunacholalamikia sisi CHADEMA na wananchi kwa ujumla, uchaguzi wa Meya wa Ilemela ulikuwa batili.
“Uchaguzi huu ulighubikwa na mizengwe mingi kwani Matata alipaswa achaguliwe na madiwani tisa, lakini akachaguliwa na madiwani sita tu.”
“Kwa maana hiyo, hatumtambui kama meya pamoja na naibu wake. Lakini Matata huyu aliwafukuza madiwani wetu watatu kinyume cha sheria na hadi sasa miezi saba wananchi wa kata hizo hawana wawakilishi na shughuli za maendeleo zimekwama,” alisema Kiwia.
Hata hivyo, aliongeza kuwa amewahi kuzungumza na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, akamhakikishia kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alishaandika barua na kuituma ofisi ya mkuu wa mkoa Mwanza kuhusu hatima ya madiwani hao, na nakala ya barua hiyo anayo waziri huyo.
Aidha diwani wa Kirumba, Dany Kahungu, alimweleza mkuu wa mkoa kuwa aliwahi kutuita ofisini kwake na kuwaonyesha barua ya Pinda yenye kurasa tatu na saini ya Waziri Mkuu dhidi yetu, hivyo akahoji iweje leo anaruka tena?
Mkuu huyo wa mkoa alikanusha kupokea barua yoyote kutoka kwa Waziri Mkuu Pinda, na alimuomba mbunge Kiwia na viongozi wengine wapande ndege kwenda Dar es Salaam kwa Waziri Mkuu Agosti 26 ili kwenda kupata ukweli wa suala hilo.
“Ofa yangu kama mkuu wa mkoa ipo wazi. Naomba Kiwia na wenzako walio tayari twendeni ofisi ya Waziri Mkuu tukakate mzizi huu wa fitina halafu turudi kuwaeleza wananchi hatima ya hili suala, kuliko wewe unaenda unakuja kusema hivi au mimi nasema hivi,” alisema Ndikilo.
RPC anena
Kuhusu ghasia zilizotokea, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alisema hakuna mtu aliyekamatwa hadi kufikia jana saa 12:15 jioni kuhusiana na vurugu hizo, na kwamba vurugu hizo hazikufanywa na wananchi wote waliokuwa kwenye maandamano hayo bali wachache ambao wanaendelea kusakwa.
Mangu alisema hakuna mtu yeyote aliyeumia wala kujeruhiwa, kwani polisi walijihami kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi kisha kufanikiwa kuwadhibiti wala hakukuwa na uharibifu wa mali uliojitokeza zaidi ya uchomaji matairi na kupangwa mawe barabarani.
|
No comments:
Post a Comment