Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Monday, August 12, 2013

CHADEMA: Tutarejesha mali zilizoporwa


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa kitapigana hadi tone la mwisho la damu kurejesha mali zote za wananchi zilizouzwa kinyemela.
Mbowe akiwa katika ziara yake kutembelea kata zote za jimbo la Hai, akiambatana na wabunge zaidi ya 11 wa chama hicho kutoka majimbo mbalimbali, alisema ili kufanikiwa katika vita hivyo, watahakikisha katiba mpya inaweka wazi ulazima wa kuanika mikataba yote ya kiuchumi iliyoingiwa na serikali.
Mwenyekiti huyo ambaye ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni alitolea mfano shamba alilopewa mwekezaji anayezalisha sukari la TPC, akisema hakuna anayejua ni kiasi gani cha fedha kinachoingia serikalini wala kilichoandikwa kwenye mkataba huo, ambao umempatia mwekezaji huyo eneo kubwa la shamba pamoja na maji huku wananchi wakitaabika kwa uhaba wa ardhi.
“Hatuwezi kuangalia mali yetu ikienda na wananchi wanataabika tukipata katiba mpya lazima mali zote zilizochukuliwa na wawekezaji mikataba irudiwe na iweke hadharani.
“Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na viwanda vingi vilivyokuwa vinafanya kazi vizuri, lakini wamepewa wawekezaji kwa sasa hakuna anayejua mkataba walioingia na serikali na viwanda vingi Moshi vimekufa,” alisema.
Alisema Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wenzake walipigana kuwaondoa Makaburu weupe na hivyo CHADEMA nao wanafanya kazi ngumu kumuondoa Kaburu weusi ili watoto wanaokuja waweze kufaidi rasilimali zilizopo nchini.
“Hivyo wananchi wangu wa Hai mkuniona niko kimya natafuta ukombozi wa nchi hii baada ya kutoka hapa nitafanya mikutano nchi nzima, lakini ninawaahidi tukimaliza Bunge la Katiba lazima nije kushinda na nyie kusikiliza zaidi kero zanu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema katiba ya sasa imetumiwa vibaya na viongozi walioko madarakani kuwalimbikizia wananchi kesi pamoja na kutowachukulia hatua viongozi wanaoiba rasilimali za umma.
Alisema wafungwa wengi magerezani ni wale wezi wadogo wadogo huku viongozi walioiba mabilioni wakiendelea kufurahia maisha uraiani.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, alisema kuwa kama kuna kiongozi wa upinzani ambaye akifa CCM watafanya sherehe ni pamoja na Mbunge wa Hai Freeman Mbowe.
Alisema Mbowe amekuwa akifanya kazi ngumu na kuleta mafanikio makubwa yakiwemo ya kuwa na wabunge wengi vijana ikiwemo yeye.
Miongoni mwa wabunge walio kwenye ziara hiyo ni pamoja na Ezeckiel Wenje, Peter Msigwa, Joshua Nasari, Lucy Owenye, Grace Kiwelu, Joseph Selasini, pamoja na madiwani wa CHADEMA kutoka Moshi, manispaa na Hai.
Wakati huo huo CHADEMA imepinga kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba kwamba hawatapokea maoni yatayopelekwa kwa njia ya Chopa.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Mabibo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema chama chao kitatumia kila njia kuwafikia Watanzania na kuwaelewesha rasimu ya Katiba mpya na msimamo wao.
Mnyika alisema kila chama cha siasa sasa kinawafikia wananchi wake, kuwaelewesha na kupata maoni yao kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya, hivyo haoni kama ni kosa kwao.
Alisema CHADEMA imeshaanza ziara na kueleza kwamba mwenyekiti wao Freeman Mbowe akishirikiana na Tundu Lissu wako mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kati huku Dk. Willibrod Slaa na Mabere Marando wakitoa elimu mikoa ya kusini na kaskazini.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo alisema wakiwa katika mchakato huo, Jaji Warioba akishirikiana na wenzake ametaka kupindisha sheria ili wampe madaraka Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa wajumbe wengine zaidi ya 100 kuingia katika Bunge la Katiba jambo ambalo CHADEMA haikubaliani nalo.
Alisema kutokana na hilo pamoja na mengine ambayo yanaweza kuchomekwa, wamemwagiza Lissu kukatiza ziara yake ili ashirikiane na wanasheria wengine kukabilina na jambo hilo.



“Baada ya kutokea dharura hiyo, nawaomba wananchi wangu nikachukue nafasi ya Lissu … nitaondoka Jumapili, nitakaa huko kwa siku 12 ili niweze kusaidiana na mwenyekiti wangu kupata maoni ya Watanzania,” alisema.
Mnyika alisema pamoja na hilo, CHADEMA imetengeneza kitabu kinachozungumzia msimamo wao kuhusu muundo wa Katiba mpya ambacho wameanza kukisambanza kwa wananchi kwa gharama ya sh 300.
Kiongozi huyo aliwataka Watanzania na Wanachadema ambao wanapenda mabadiliko kukinunua kwa ajili ya kupata uelewa kuhusu rasimu hiyo na nini wanapaswa kuchangia.
Wakati huohuo, Mnyika aliwataka wananchi na Wanachadema kumchagua mgombea uenyekiti wa mtaa wa Sahara Relini Mayunga Kadwisha katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho Agosti 11, mwaka huu.
Akimnadi mgombea huyo, Mnyika alisema nchi hii inapaswa kuongozwa na mtu anayependa mabadiliko hasa CHADEMA na si vinginevyo.
‘Wananchi wa Sahara na Reline, mchagueni Kadwisha siku ya Jumapili kwa ajili ya maendeleo ya mtaa wenu … hakuna mgombea mwingine, na hapa nafikiri kama CHADEMA isingemweka mgombea huyu likawepo jiwe, mngechagua jiwe kuliko CCM,” alisema Mnyika.

No comments:

Post a Comment