CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesisitiza kuwa sheria ya
mabadiliko ya Katiba mpya ndiyo inavyowaruhusu kukusanya maoni wala si
utashi wa mtu.
Akizungumza
jijini Arusha juzi katika kikao cha baraza la kitaasisi la kukusanya
maoni ya kuboresha rasimu ya Katiba mpya yanayoratibiwa na chama hicho,
Mjumbe wa Kamati Kuu, Mabere Marando, alisema wako sahihi.
“Kifungu cha
18 (1) (2) cha sheria ya mabadiliko ya Katiba ndicho kinaagiza hivyo
wala si utashi wa mtu,” alisema Marando katika viwanja Kilombero kwenye
mkutano aliohutubia pia na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.
Alisema kuwa
kifungu hicho cha sheria ya marekebisho ya Katiba mpya, kinavitambua
vyama vya siasa kama taasisi na hivyo kuweza kutoa mapendekezo ya maoni
ya rasimu ya Katiba sawa na mabaraza ya wilaya.
“Wananchi endeleeni kutoa maoni yenu nawahakikishia Jaji Warioba apende asipende ni lazima ayapokee mapendekezo haya,” alisema.
Marando
alitaja mambo manne makuu wanayoyataka yaingie kwenye Katiba kuwa ni
suala la Tume Huru ya Uchaguzi ambapo Rais anyang’anywe mamlaka ya
kuteua mwenyekiti wa tume hiyo na wajumbe wake.
“Tunaunga
mkono mapendekezo ya rasimu ya Katiba ya kutaka wajumbe hao waombe
nafasi hizo, wadahiliwe na kuthibitishwa na Bunge kisha majina yapelekwe
kwa Rais ambaye atayatakangaza bila kufanya marekebisho yoyote,”
alisisitiza.
Marando
alisema kuwa wanapendekeza uwepo uwazi kwenye uendeshaji wa serikali
hasa kwenye masuala ya mikataba ambayo kwa muda mrefu imefanywa siri na
hivyo kupora rasilimali za taifa.
Naye Dk.
Slaa aliitaka CCM kuacha unafiki wa kudai kwamba serikali tatu itaongeza
gharama za uendeshaji, na kusisitiza kuwa kama wanataka kupunguza
gharama wangependekeza serikali moja.
Alitoa mfano
akisema kuwa muundo wa sasa wa serikali mbili idadi ya wabunge wote
pamoja na wawakilishi ni 438 wakati kwa muundo wa serikali tatu idadi
itapungua na kubaki 314.
Dk. Slaa
alisema kuwa ni vema Rais na watumishi wote wa umma waondolewe kinga ya
kutoshtakiwa pindi wakiwa na wakitoka madarakani ili kuongeza
uwajibikaji.
Wakati huo
huo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph
Warioba, ameendelea kuzitaka taasisi mbalimblai kuacha kuwashawishi
maoni wafuasi wao katika mchakato wa kujadili rasimu.
Akizungumza
mjini Dodoma jana baada ya ufunguzi wa utoaji wa maoni katika mabaraza
kwa watu wenye ulemavu, alisema kuwa kuna matatizo makubwa ambayo
yanaonekana kujitokeza nchi nzima kwa taasisi mbalimbali kuwatumia
wananchi kutoa maoni kwa maslahi yao.
“Wajumbe
wameanza kuingiliwa na taasisisi mbalimbali pamoja na baadhi ya viongozi
wa vyama vya siasa badala ya kuwaacha kutoa maoni yao,” alisema.
Kuhusu suala la serikali tatu, alisema kuwa Watanzania wasiwe na wasiwasi kwa kudhani kuwa itakuwa na gharama kubwa.
No comments:
Post a Comment