MWENYEKITI na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wanaanza rasmi ziara nchi nzima kwa kutumia helikopta kwa ajili ya kuzindua mabaraza ya Katiba ya chama.
Ziara hizo zitakazowashirikisha wabunge wote na viongozi wengine zinaanza rasmi leo, ambapo mwenyekiti Freeman Mbowe atazindua mpango huo mkoani Mara.
Wakati Mbowe akianzia mkoani Mara, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa atakuwa mkoani Tanga kuanzia Agosti 15 na kuendekea katika mikoa mingine.
Taarifa kutoka ndani ya CHADEMA zinasema kuwa viongozi hao watapita katika kila jimbo la uchaguzi ambapo kila mkoa watakaa siku zisizopungua nne wakijadili rasimu hiyo ya Katiba na wafuasi wao.
Kutoka mkoani Mara, mwandishi wetu anaripoti kuwa wakazi wa Tarime wamemwandalia mapokezi makubwa Mbowe ambaye atawasili wilayani humo kesho alasiri akitokea Serengeti.
Mwenyekiti wa madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Charles Mbusiro, aliliambia gazeti hili kuwa wamejiandaa vyema kumpokea kiongozi huyo.
Alisema kuwa Mbowe na timu yake watazungumzia juu ya mchakato wa Katiba mpya unaoendelea kwenye rasimu pamoja na hati iliyozuiliwa kwa ajili ya kuzinduliwa halmashauri ya mji wa Tarime iliyoanza kufanya kazi Julai mosi mwaka huu.
Aliongeza kuwa Mbowe atafuatana na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu, Prof. Abdallah Safari na viongozi wengine.
Wakati Mbowe akianza mashambulizi hayo kanda ya Ziwa, Dk. Slaa na viongozi wengine wataanzia Kanda ya Kaskazini kwenye mkoa wa Tanga.
Kwa mujibu wa Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje, Dk.Slaa atafanya mikutano ya hadhara katika wilaya zote za mkoa huo akizungumzia rasimu ya Katiba mpya.
Kama itakavyokuwa kwa Mbowe, pia Dk. Slaa naye atatumia usafiri wa helikopta katika kuzitembelea wilaya hizo za Lushoto, Handeni, Korogwe, Muheza na Tanga mjini.
Bahweje alisema kuwa chama hicho ngazi ya mkoa kinaendelea na mikutano ya hadhara na ya ndani kwa lengo la kuelezea mkakati wake.
Katika hatua nyingine, Mbowe amesema hana mpango wa kuliacha jimbo lake la Hai kwa ajili ya kwenda kugombea ubunge Moshi Mjini kama anavyozushiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mbowe alitoa kauli hiyo baada ya kukuwepo na taarifa kuwa katika uchaguzi ujao atagombea ubunge Moshi mjini, jimbo ambalo kwa sasa linaongozwa na Philemon Ndesamburo (CHADEMA).
Akizungumza na wananchi wa kata ya Hai mjini juzi, Mbowe alisema hana mpango wa kuliacha jimbo hilo na kwamba uvumi unaosambazwa ni kuwatia hofu wananchi.
“Wananchi wa Hai nimepata taarifa kuwa kuna maneno yanaenezwa na CCM kwamba nina mpango wa kuwaacha wananchi wangu na kwenda kugombea Moshi mjini au Dar es Salaam, naomba niseme kuwa taarifa hizo si sahihi nitaendelea kuwatumikia hadi mtakapoamua nyie.”
“Nimetembea na wabunge wenzangu kwenye kata mbalimbali za jimbo langu, tumesikiliza kero zenu lakini wabunge wamefurahishwa na jinsi wananchi wangu wanavyoniita kaka na mimi nawaambia CCM hili ni jimbo la kaka,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbowe alitangaza vita na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga, pamoja na Katibu wa CCM wilaya, Hassan Mtenga, kwa kile alichoeleza kuwa ni kwa kufanya siasa zisizo za kistaarabu.
Mbowe alizungumzia suala la uwanja wa Sabasaba uliokuwa ukimilikiwa na halmashauri kutaifishwa na kuzuia mikutano ya upinzani isifanyike hapo.
“Hatuwezi kuwa watumwa ndani ya nchi yetu, uwanja wanaoita wa CCM ulikuwa ni wa halmashauri na ni wa Watanzania wote hakuna haja ya kuukumbatia uwanja huo na sisi kufanyia mikutano standi,” alisema.
No comments:
Post a Comment