CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo [Chadema] kinakusudia kuwafikia na kukusanya maoni kuhusu katiba mpya, Watanzania milioni tano katika wiki mbili zijazo. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikuwa aizungumza na wananchi mjini Nansio katika Wilaya ya Ukerewe.
Akihutubia mamia ya wananchi katika uwanja wa Mongera , alisema Chadema imechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya imefikia idadi ndogo ya watanzania.
Mbowe alisema katika miezi sita tume hiyo imekusanya maoni ya watu 18,000 kwa gharama ya Sh bilioni 20.
Alisema yeye na Katibu Mkuu wake, Dk. Willbrod Slaa wamejigawa katika makundi mawili wakiongoza viongozi wa wengine wa chama hicho kukusanya maoni nchi nzima.
Naye Beatrice Mosses kutoka Babati anaripoti kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa ameitaka Serikali kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Katiba ya kubadilisha daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuandikishwa majina upya watanzania wengi wapate haki ya kupiga kura.
Alikuwa akizungumza katika mkutano wa kupokea maoni ya katiba mpya kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati mkoani Manyara.
"Hivi sasa kila mahali unapofanyika uchaguzi mdogo idadi ya watu wanaojitokeza kupiga kura inapungua kwa sababu wengi wao wamefikia umri wa kupiga kura na wengine wamepoteza vitambulisho hivyo kukosa haki zao," alisema Dk. Slaa.
Alisema Serikali isikilize maoni ya tume kwa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuagiza hatua hiyo kufanyika upya.
Source: Mtanzania
No comments:
Post a Comment