Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Saturday, June 18, 2011

Wabunge, waziri watunishiana misuli

* Ni Kabaka, Jenista Mhagama, Mbilinyi (Sugu)
* Wavutana katika kutembelea kiwanda
* Kiwandani wabunge washuhudia ‘madudu’
* Wafanyakazi wanalazimishwa kuvaa kaptura
* Wabunge watokwa machozi kwa waliyoyaona


Na Arodia Peter
Dar es Salaam


WAZIRI wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Gaudensia Kabaka jana alivutana vikali na wabunge wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii waliokuwa wanataka kutembelea Kiwanda cha Vyombo vya Nyumbani cha Jambo Plastiki kilichoko Dar es Salaam.
Wakati wajumbe wa Kamati hiyo wakiwa wamekwisha kujiandaa kwenda katika kiwanda hicho jana, ghafla Waziri Kabaka aliwaeleza kuwa ziara hiyo imeahirishwa hadi wakati mwingine.
Kabaka alitoa sababu za kutaka kuahirisha ziara hiyo kuwa ni mgogoro wa wafanyakazi na mwajiri kiwandani hapo ambao upo mahakamani hivyo ziara hiyo itakuwa ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Baada ya kutolewa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jenista Mhagama alikuja juu na kumweleza Kabaka kuwa kamwe kamati yake haiwezi kuahirisha ziara hiyo bila kutolewa sababu za kuridhisha. Alisema kitendo alichokifanya Waziri kinadhalilisha kamati yake.
“Mheshimiwa Waziri kitendo ulichokifanya unaingiza mgogoro mkubwa katika kamati ya Bunge… kwa mazingira ya sasa Watanzania hawana mahali popote pa kutolea shida zao zaidi ya bunge na hii inadhihirika wazi wataalamu wako hawakukushauri vizuri,” alisema Mbunge huyo wa Peramiho kwa tiketi ya CCM na kuongeza:
“Basi kama ni hivyo, Mheshimiwa Waziri mimi nakupisha uwe mwenyekiti wa kamati ya Bunge maana naona hutaki kutuelewa.”
Kuona hivyo, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwa uzoefu uliopo nchini unaonyesha kuwa ziara hiyo tayari imekwicha kuchakachuliwa na wahusika kwa manufaa wanayoyajua wao.
Alisisitiza kwamba kama ziara itaahirishwa basi yeye hatakuwamo kwenye orodha hiyo.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) alisema kama kamati haitaki kwenda kwenye kiwanda hicho yeye atapanga ziara yake kama mbunge wa Chadema na kwenda kusikiliza na kukagua mazingira kiwandani hapo.
Asumpta Nshunju (CCM) ambaye ni Mbunge wa Nkenge, alisema kuna dalili za wazi watu wamepokea chochote kutoka kwa mwekezaji ndiyo maana kamati imepigwa ‘stop’ dakika za mwisho.
Akimsaidia waziri wake, Ofisa Kazi Mfawidhi wa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Josephat Rugakingira aliwaambia wabunge kwamba haingekuwa vizuri kutembelea kiwanda hicho wakati mgogoro kati ya menejimenti na wafanyakazi bado uko Baraza la Usuluhishi wa Migogogro (CMA) ikiwa imefunguliwa kesi namba DMA/DSM/ILALA/ 2009.
Hata hivyo baada ya mvutano mkali hatimaye Waziri Kabaka alikubaliana na wabunge na kuamua kufanya ziara kiwandani hapo wakati huo ikiwa saa 7.00 mchana.
Kiwandani
Wabunge walipofika kiwandani walipangua ratiba iliyokuwa imeandaliwa iliyotaka wafanyakazi na menejimenti kukutana na kamati ya Bunge kwa pamoja.
Kamati ya Bunge iliamua kukutana na wafanyakazi pekee, kikao kilichodumu kwa zaidi ya saa moja. Waandishi wa habari wa menejimenti hawakuruhusiwa katika kikao hicho.
Baada ya kumalizika kikao hicho, wabunge walitoka nje wakiwa wanafuta machozi na baadhi yao walisema waliingiwa na simanzi kubwa kutokana na mambo mazito waliyoelezwa katika kikao hicho.
Hata hivyo, ilibainika kuwa katika kikao hicho ambacho Waziri pia alishiriki, kesi iliyokuwa inasemwa kuwa ipo mahakamani haikuwa kweli kwa vile ilikwisha kutolewa uamuzi tangu mwaka 2009.
“Hii kama siyo rushwa ni nini, ndiyo maana walitaka kutuchakachua tusije hapa kwa maslahi yao, hii ni aibu. Wataalamu wa Wizara ndiyo wanaotufanya sisi wabunge wa CCM tuonekane hatuna thamani mbele ya umma… kumbe ni watu wachache waliojiwekea mtandao wa rushwa kwa njia wanazozijua wao,” alisema mmoja wa wabunge kwa sharti la kutotajwa jina.
Waziri Kabaka akiri, aiomba radhi kamati
Baadaye Waziri Kabaka aliomba radhi kwa Kamati ya Bunge kutokana na hali iliyojitokeza awali. Alisema yeye hakujua kama alichoambiwa na wataalamu wa Wizara yake kilikuwa ni uongo na uzushi.
“Mheshimiwa mwenyekiti naomba radhi kwa yaliyotokea, nakiri nilidanganywa sasa nimejifunza kutoka kwenu,” alisema Kabaka kwa sauti ya upole.
Alipoulizwa na waandishi wa habari ni hatua gani atawachukulia wataalamu waliomdang’anya, alisema:
“Niachieni nitashughulika nao, tutaongea na wenzangu tuone ni kwa nini wamefanya hivyo”.
Wafanyakazi wanalazimishwa kuvaa kaptura
Kiwandani hapo wabunge walishuhudia wafanyakazi wakike na kiume wakiwa wamevaa kaptura na fulana ikiwa ndiyo sare za kiwanda hicho.
Wakizungumzia hali hiyo baadhi ya wafanyakazi walisema hawaruhusiwi kuvaa nguo tofauti na hizo kiasi kwamba wakati wa baridi wanapata shidakubwa lakini hawana la kufanya.
“Hizi ndiyo nguo zetu rasmi hapa kazini. Tukivaa tofauti na hizi tunafukuzwa kazi, tunashukuru mmekuja wabunge wetu mtutetee tunaangamia,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Kwenye mgahawa wa wafanyakazi, hali pia ni mbaya na wabunge walishuhudia uchafu uliokithiri huku vyombo vya kulia chakula vikiwa vya plastiki jambo ambalo ni hatari kwa afya za wafanyakazi hao.
Baadhi ya wafanyakazi walisema licha ya kutumia vyombo vya plastiki pia wanalazimika kutumia vikombe kwa kupokezana kwa vile vilivyopo havitoshi.
“Hata sisi tunaonekana kana mbwa, angalieni sehemu hii tunayolia chakula. Haifai hata kwa mnyama mbwa maana ni chafu kupindukia lakini hawatujali,” walisema baadhi ya wafanyakazi.
Wafanyakazi wa kigeni
Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Manoj Suchak aliulizwa kuhusu hatua ya kuajiri wafanyakazi wa kigeni katika nafasi zote za juu bila kuhusisha mfanyakazi mzawa hata mmoja.
Akijibu swali hilo lililoulizwa na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), alisema kati ya mameneja saba wa kiwanda hicho ni watano tu ambao ni wazawa.
Hata hivyo Nkamia alipotaka amwone angalau mmoja ambaye ni mzawa, alitokea kijana mwenye asili ya Asia, jambo lililozua kicheko na miguno kutoka kwa wabunge.
Ziara hiyo ya wabunge ilikuwa pamoja na mambo mengine kukagua mazingira ya kiwanda, kusikiliza mgogoro baina ya wafanyakazi na manejimenti ya kiwanda hicho ambao umedumu kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment