Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Saturday, April 9, 2011

Studio ya JK yazua mjadala bungeni


na Bakari Kimwanga, Dodoma

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), jana iliibuka bungeni na kudai studio iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kukuza vipaji kwa wasanii nchini wamepewa watu ambao hawana msaada kwa wasanii na hata chombo kinachoisimamia hakijasajiliwa.
Akiuliza swali la nyongeza baada ya lile la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata, aliyetaka kujua wasanii wamenufaikaje na mtambo huo wa studio uliotolewa na Rais Kikwete, Mbilinyi maarufu kama ‘Mr II au Sugu’, alihoji kutokana na hali hiyo kwa nini serikali imekuwa inapata kigugumizi kulipa mamlaka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili kuiendesha kikiwa ni chombo ambacho kinasimamia maslahi ya wasanii wote nchini.
“Mheshimiwa Spika ninazungumza kwa niaba ya wasanii wa hapa nchini, hakika hiki chombo kinachoitwa Tanzania Flava Unit hakijasajiliwa na hata BASATA waligoma kukisajili kutokana na kazi zake kufanana na Chama cha Wanamuziki wa Muziki wa Kizazi Kipya nchini, sasa serikali haioni haja ya kuipa BASATA kusimamia studio hii?” alihoji Sugu.
Aidha aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wasanii nchini kuhusu studio hiyo kutowasaidia na hata kushindwa kurekodi nyimbo zao.
Swali hilo lilimuinua Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, ambapo alijibua kuwa hakuna sheria inayozuia kusajiliwa kwa Tanzania Flava Unit kama kazi ya kusimamia studio hiyo iko sahihi, huku Baraza la Sanaa akiahidi kutafutiwa kazi nyingine.
Awali akijibu swali la msingi, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alisema, ‘Mastering Studio’ iliyotolewa na rais, haikutolewa kwa kituo cha radio cha Clouds FM, bali imetolewa kwa kikundi cha wasanii waliojiunga pamoja na kuanzisha Chama cha Tanzania Flava Unit.
Alisema wasanii hao ni wale wa Tanzania House of Talent (THT), na baadhi ya wanamuziki wa kizazi kipya ambao wana ushirikiano wa karibu sana wa kiutendaji kazi na kituo cha Radio Clouds FM kinachoongozwa na Ruge Mutahaba na bado haijaanza kufanya kazi, hivyo ni mapema kueleza ni wasanii wangapi wamenufaika.

No comments:

Post a Comment