Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Wednesday, April 6, 2011

Siku Mhe. Joseph Mbilinyi Alipotembelea Jukwaa La Sanaa

Mbunge wa Mbeya Mjini Mh. Joseph Mbilinyi maarufu kwa Jina la Sugu akiongea na wadau wa Jukwaa la Sanaa jana wakati alipohudhuria kwa mara ya kwanza toka achaguliwe kuwa mbunge. Sugu ni moja ya wadau wa Jukwaa hilo linalofanyika kila Jumatatu Ukumbi wa BASATA.
 
Profesa Amandina Lihamba kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichokoza mada kuhusu tasnia ya Filamu hapa nchini kwenye Jukwaa la Sanaa BASATA jana. Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego.

Na Mwandishi Wetu:
Jukwaa la Sanaa BASATA limempongeza kwa ushindi wa ubunge na kumpa kazi ya kutetea maslahi ya wasanii Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni mmoja wa waasisi wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina Sugu.


Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye ukumbi wa BASATA kwa niaba ya wadau wote. Profesa Amandina Lihamba kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye alikuwa ni Mratibu wa Jukwaa hilo alisema kwamba, wadau wa Jukwaa la Sanaa wanampongeza kwa dhati kwa ushindi wake na wanamtuma bungeni kutetea haki zao na kwamba asiwatupe.


“Tunajua toka ushinde leo ni mara yako ya kwanza kuonana na hadhira ya wasanii hivyo tunachukua fursa hii kukupongeza kwa dhati, uendelee na moyo huo huo wa kuwapigania wasanii na usiwatupe” aliongeza Profesa Lihamba.


Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema kwamba, pamoja na BASATA awali kutuma barua ya pongezi kwake na kwa wabunge wengine wasanii, bado Jukwaa la Sanaa lina kila sababu ya kumpongeza na kumtuma kwenda kutetea haki za wasanii na kuhakikisha maslahi ya sekta ya sanaa yanalindwa.


“Naomba niungane na wenzangu kutambua uwepo wa Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini, msanii mwenzetu naimani sasa tunapozungumza hapa katika Jukwaa tunazungumza na mtu ambaye sasa atakuwa bungeni akiwakilisha wasanii. Pamoja na barua ya kumpongeza tuliyomtumia yeye na wasanii wengine walioingia bungeni, tunampongeza tena kwa dhati” alisema Materego.


Naye Mbilinyi aliyeambatana na Katibu wake Fred Maliki, maarufu kwa jina la usanii la Mkoloni alimshukuru Materego kwa pongezi zake lakini akapongeza juhudi anazochukua katika kuwahabarisha na kuwapa fursa ya elimu wadau wa sanaa. Aliahidi kuendeleza harakati za kupigania haki za wasanii kwani ndicho kitu ambacho ataanza nacho.


“Harakati za kupigania haki za wasanii nimezianza kwa muda mrefu nawaahidi kwamba sitarudi nyuma na kwa sasa napenda niwaambie kwamba, mapambano ndiyo kwanza yameanza kwani sasa ndiyo tumekabidhiwa rungu” alimalizia Mbilinyi ambaye aliwahi kutamba na nyimbo kama za Mikononi mwa polisi, Deiwaka, Dar moto chini, Wananiita Sugu, Hold On na nyingine nyingi.

No comments:

Post a Comment