Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Wednesday, April 6, 2011

Mbunge Joseph Mbilinyi apinga kiwanda kugeuzwa ghala la bia.

Na Joachim
Nyambo,Mbeya

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Mr II, amesema
kitendo cha serikali mkoani hapa kukabidhi majengo ya kilichokuwa
kiwanda cha zana za kilimo (ZZK) yaliyopo eneo la Iyunga jijini hapa
kwa kampuni ya vinywaji ya TBL yatumike kama maghala kinakinzana na
mpango wa serikali wa kufufua viwanda muhimu kama hicho.

Mhe. Joseph Mbilinyi (Sugu) akiwa katika moja ya mikutano yake

Kabla ya kusimamisha uzalishaji wa zana zaidi ya miaka kumi iliyopita
hali iliyosababishwa na mwekezaji aliyekabidhiwa kushindwa kukiendesha
kiwanda hicho kilikuwa tegemeo kubwa la wananchi wa mkoa wa Mbeya
ambao asilimia yao kubwea ni wakulima.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa kata za Nsalaga na Uyole  katika
viwanja vya kibonde Nyasi, Mbunge huyo amesema hatua hiyo moja kwa
moja imewapa hofu wananchi kuwa huenda serikali haina mpango tena wa
kukifufua ili kiendelee na uzalishaji wa zana hizo ambao utaweza
kuwapunguzuia gharama za ununuzi wa pembejeo tofauti na ilivyo hivi
sasa.
Amesema  inashangaza kuona kuwa baadhi ya watendaji wa serikali ambayo
kila siku inahubiri mpango wa kukuza uchumi wa wananchi wake kupitia
kilimo kwa sera mbalimbali ikiwemo Kilimo Kwanza wanakubali kumpa
mwekezaji ambaye anayegeuza kiwanda cha ZZK kuwa ghala la kuhifadhia
bia.
Amesema wananchi wa mkoa wa Mbeya kwa ujumla walikitegemea sana
kiwanda hicho kiweze kufufuliwa na kuzalisha zana za kilimo ambazo
zingepatikana kwa urahisi kwani zingeuzwa kwa bei ndogo kwa wakulima
ili waweze kuboresha kilimo chao lakini sasa matumaini yao yameanza
kufifia.
Mbilinyi amesema kama kiwanda hicho kingefufuliwa hata Trekta ndogo
aina ya Powertiller zinazoagizwa nje ya nchi kwa bei kubwa zingeweza
kuzalishwa katika kiwanda hicho na kuuzwa kwa bei ambayo wakulima
wangemudu kununua.
Hata hivyo Mbilinyi amesema yupo tayari kubisha hodi katika ofizi za
Waziri wa Viwanda ili apewe maelezo ya kina juu ya mwongozo uliotumika
kwa serikali kugeuza kiwanda hicho kuwa ghala la kuhifadhia bia badala
ya kuweka mikakati ya kukifufua.
Aidha Mbunge huyo amepongeza hatua ya seriakali kujenga uwanja wa
ndege wa Songwe , akisema ameridhishwa hatua za ujenzi zinazoendelea
baada ya kuutembelea na kuelezwa na wataalamu kuwa ifikapo Agosti
mwaka huu ndege zitakuwa zimeanza kutua katika uwanja huo.
Mbilinyi amesema kukamilika kwa uwanja huo ni changamoto kubwa ya
maendeleo katika mkoa wa Mbeya na kuwataka wananchi kujiandaa vyema
kuutumia uwanja huo kwa manufaa hususani kwa kuzalisha mazao
yanayoweza kusafirishwa nje ya nchi na kuuzwa kwa bei yenye kuwaletea
tija.

No comments:

Post a Comment