Tuko Pamoja

Tuko Pamoja

Thursday, August 15, 2013

Mbowe: Katiba Mpya inahitaji hekima, busara

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema, kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kupata Katiba Mpya siyo kazi rahisi, ni kazi inayohitaji nia ya dhati ya taifa zima, kwa kuwa katiba ni mali ya wananchi na rasilimali za taifa.
Mbowe alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara wa kukujadili Rasimu ya Maoni ya Katiba, uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo wilayani Musoma Mkoa wa Mara hivi karibuni.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa kazi hiyo, Chadema wameamua kuzunguka nchi nzima kwa lengo la kutoa elimu ya Katiba kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kutoa ufafanuzi wa maana ya Katiba na kujibu hoja za wananchi hao.
Alisema kuwa Tanzania ambayo ilikuwa ikisifika kama nchi ya amani na mshikamano kwa miaka mingi, sasa inaelekea kubomoka na hali hiyo inatokana na katiba mbovu isiyokuwa na mipaka ya madaraka ambayo sasa tumeamua kuifanyia mabadiliko.
“Hebu angalieni sasa hivi kuna ugomvi wa dini, wananchi na Serikali hususan katika maeneo yaliyo na madini, vyombo vya usalama na raia na mengine mengi. Je hii ndiyo Tanzania yenye amani na mshikamano aliyoiacha Hayati Baba wa Taifa?” alihoji Mbowe.
Alisema katika kuzungumzia Katiba hakuna vyama vya siasa, polisi wala mtu wa kada nyingine yoyote. Katiba ni mali ya Watanzania wote, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutoa maoni yake juu ya mambo anayoamini kuwa yatalisaidia taifa kama yataingizwa kwenye katiba.
Awali akihutubia katika mkutano huo,Mmbunge wa Ubungo John Mnyika, alisema kuwa maadili ya uongozi na utawala bora, vinatikiswa kama siyo kuyumbishwa. Aliwataka wananchi kuhakikisha misingi ya taifa inarekebika kupitia marekebisho ya katiba mpya.
Mnyika alisema kuwa katika kupitisha maoni ya katiba, wanataka haki, uwazi na usawa katika masuala ya madini na rasilimali za nchi ambazo kimsingi zinapaswa kutajwa kwenye katiba. Tunataka Katiba pia impunguzie rais madaraka, alisema.
Alisema gharama za maisha ya wananchi zinazidi kupanda kila kukicha kutokana na rais kuwa na mlimbikano wa madaraka, hivyo kufanya maamuzi bila kutambua kuwa wananchi walio na kima cha chini ndio wanaoumia.
Aidha alisema kuwa anashangazwa na serikali ya CCM inavyokataa mfumo wa serikali tatu kwa madai kuwa,serikali tatu ni gharama kubwa sana kuendesha huku wakisahau baraza kubwa la mawaziri lisilo na meno.
Chadema imekuwa ikifanya mikutano ya hadharani nchini kuzungumzia mchakato wa katiba. Wamekuwa wakitoa elimu na kuwaeleza wananchi umuhimu wa kazi hiyo kwa taifa.

Wednesday, August 14, 2013

Muungano wazua mjadala Mwanza


Wajumbe wa Baraza la Katiba wilayani Nyamagana, wamechafua hali ya hewa na kumweka mwenyekiti wa baraza hilo, Muhamed Mshamba katika wakati mgumu baada ya kuibuka makundi mawili yaliyokuwa yakivutana kuhusu Muundo wa Muungano.
Wakati kundi moja likiwa linatetea Muundo wa Serikali mbili, lingine likataka Serikali tatu. Kundi linalotaka Serikali tatu limeeleza kuwa Serikali mbili kufanya kazi ilizotumwa za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Akichangia hoja hiyo, mwakilishi wa wananchi wa Kapripot, Milton Rutabana alisema kuwa, Muungano wa Serikali mbili umeshindwa kutatua kero nyingi,  ikiwemo fursa za maendeleo katika nyanja za uchumi, siasa na jamii.
Alisema kuwa Serikali mbili za Muungano zimekiuka makubalianao yaliyowekwa kwenye hati ya Muungano ya mwaka 1964. “Ilitakiwa kuwa na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika, Jamhuri ya watu wa Zanzibar kwa jina la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema.
Aliendelea kufafanua na kudai kuwa mambo ya Muungano yalikuwa mawili tu mwaka huo wa 1964, lakini sasa hivi yameongezeka na kufikia mambo 22 bila ya ridhaa ya wananchi kutoka pande zote mbili za Muungano.
Hoja hiyo ya Rutabana ilizua  vurugu katika kikao hicho baada ya upande wa pili kuona kuwa wanazidiwa hoja katika kutetea Serikali mbili na kudai kuwa ili waweze kukubali Serikali tatu, Tume ihakikishe inapata hati halisi ya makubaliano ya Muungano ili waweze kufanya uamuzi.
Rutabana aliendelea kueleza kuwa Serikali za Muungano kwa jina la Tanzania imeinyima utambulisho nchi ya Zanziabar na hivyo kuifanya isiweze katika vikao vya kimataifa ikiwamo vya UN, OIC, Fifa na E.A.C.
“Ni muhimu sasa kuwepo na Serikali tatu ili tupate sehemu ya kupeleka malalamiko yetu ya kimaendeleo kama Serikali ya Zanzibar ilivyo na Rais wake, bendera yake na wimbo wake wa Taifa,” alisema Rutabana na kuongeza;
Mjumbe wa baraza hilo kutoka Igoma Adamu Chagulani, alidai kuwa Serikali mbili za Muungano zimekuwa kikwazo kikubwa cha kutatua kero za Muungano, ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu huku wabunge wa Zanzibar wamekuwa wakitunga sheria au kukataa sheria kwa mambo ambayo ni ya Muungano.
Alisema kuwa kuna haja ya kurejea matakwa ya kuwa na Serikali tatu kama historia ndefu inavyojionyesha hali iliyopelekea baadhi ya watu kujazwa chuki baada ya kudai Serikali tatu.
Alisema kuwa kuanzia kwa utawala wa Abdu Jumbe mwaka 1984 Zanzibar kulichafuka sababu hiyo ya Serikali tatu, mwaka 1990, G55 wabunge walidai kuwe na Serikali tatu na madai hayo yalikuwa chini ya Waziri mkuu Malecela na baba wa Taifa alifanikiwa kuzimisha.
“Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 ilitaka Serikali tatu, Tume ya Jaji Kisanga 1998 ilitaka Serikali tatu, Tume ya Jaji Warioba 2012 nayo imekuja na majibu hayo hayo,” alisema Changulani.

 UZEMBE WA TANESCO WASABABISHA KIFO CHA BINTI WA MIAKA 26 JIONI HII MBALIZI MBEYA.



 HAPA NDIPO MAREHEMU ALIPOGUSA NA KUKUTWA NA MAUTI

NYAYA ZA UMEME AMBAZO ZIMENING'INIA MITA MOJA KUTOKA USAWA WA ARDHI ZIMESABABISHA KIFO CHA NEEMA B. KIPENYA (26) ALIPOTELEZA NA KUKAMATA NYAYA HIZO KISHA KUFARIKI PAPO HAPO.
 KATI YA NGUZO HADI NGUZO NI UMBALI WA ZAIDI YA MITA 75 MAHALI AMBAPO PALIPASWA KUWA NA NGUZO TATU LAKINI IKAWEKWA NGUZO MOJA , HALI MTEJA WA ENEO HILO ALIKUWA AMELIPIA NGOZO TATU ZAIDI YA MIAKA MIWILI ILIYOPITA .
 HAPA NDIPO ALIPO TELEZA MAREHEMU NEEMA NA KUANGUKIA NGUZO HIZO



 ASKARI AKIPATA MAELEZO KUTOKA KWA MASHUHUDA 
 MWENYEKITI WA KIJIJI CHA MSHIKAMANO BWANA KISMAN MWANGOMALE AMBAYE NDIYE MTEJA WA KWANZA KULIPIA TANESCO NGUZO TATU  NA KUFUNGWA NGUZO MOJA , NA AMETOA TAARIFA MARA KADHAA TANESCO NA HATA KUANDIKA BARUA KWA NIABA YA KIJIJI LAKINI HAKUNA UTEKELEZAJI ULIOFANYIKA HADI MADHARA YAMETOKEA NDIPO TANESCO WAMEFIKA.

MMOJA KATI YA WATUMISHI WA TANESCO AMBAYE ALIFIKA ENEO LA TUKIO NA KUKATA UMEME USILETE MADHARA ENEO HILO , HATA HIVYO ALINUSURIKA KUPIGWA NA WANANCHI WENYE HASIRA KALI AMBAO WALIKERWA NA TUKIO HILO.

 MWENYEKITI WA KIJIJI CHA MSHIKAMANO WA KWANZA KUSHOTO NA WATUMISHI WA TANESCO WAKIANGALIA NGUZO ZILIZO ELEMEWA NA UZITO WA NYAYA HIZO NA KUSABABISHA NGUZO KUSHINDWA KUHIMILI UZITO WA NYAYA HIZO. 
 WAOMBOLEZAJI WAKILIA KWA UCHUNGU KWANI MUDA MFUPI ULIOPITA WALIKUWA NA MAREHEMU NYUMBANI HAPO.
 

PICHA NA EZEKIEL KAMANGA
NA MBEYA YETU BLOG
 
Chanzo: Mbeya Yetu Blog

CCM kwachafuka: RUSHWA, MIZENGWE VYATAWALA KUMBEBA MEYA, kimewafukuza uanachama madiwani wake wanane

 
HATIMAYE Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera kimewafukuza uanachama madiwani wake wanane, waliokuwa wamesaini hati ya tuhuma za ufisadi, ili kumng’oa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
Hata hivyo, uamuzi huo unadaiwa kulinda ufisadi anaotuhumiwa kufanywa na Amani katika utekelezaji wa miradi mitatu ya upimaji viwanja, ujenzi wa soko la kisasa na kituo cha mabasi.
Madiwani hao wanane pamoja na wenzao saba wa CHADEMA na CUF walisaini hati ya kutokuwa na imani na meya huyo na kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kumng’oa tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Waliofukuzwa na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni naibu meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
Wapinzani waliokuwa wameungana nao ni Dismas Rutagwelela (Rwamisenyi), Israel Mlaki (Kibeta), Winfrida Mukono (viti maalumu), Conchester Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu CHADEMA pamoja na Ibrahim Mabruk (Bilele), Felician Bigambo (Bakoba) na Rabia Badru (viti maalumu - CUF).
Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa vikali na baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanaamini kwamba kufukuzwa kwa madiwani hao ndilo kaburi la chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.
“Sijawahi kuona ujinga wa namna hii. Huwezi kufukuza madiwani wanane kwa wakati mmoja halafu chama kikabaki imara,” alisema mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM alipohojiwa na Tanzania Daima Jumatano.

 Mkakati wa kuwafukuza madiwani hao ulidaiwa kutawaliwa na vitendo vya rushwa na mizengwe ndani ya CCM, vilivyodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa chama na serikali Mkoa wa Kagera kwa lengo la kumwokoa meya.
Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kagera, Hamimu Mahamud, kura za ndiyo zilikuwa 50 wakati zile za hapana zilikuwa tano.
Hata hivyo, madiwani hao waliovuliwa uanachama walidai kuwa Halmashauri Kuu (NEC) haina mamlaka ya kuwachukulia hatua hizo bali uamuzi huo ulipaswa kupitia NEC wilaya baada ya kujadiliwa na sekretarieti na kamati ya siasa.
Awali katika kuwadhibiti madiwani hao ili wasitimize lengo lao, kutwa nzima ya jana CCM ilifanya vikao viwili vya Kamati ya Siasa na NEC mkoa ili kuwajadili.
Vikao hivyo ni mwendelezo wa vile vitatu vya sekretarieti, kamati ya siasa na NEC vilivyomalizika wiki iliyopita pasipo kufikia muafaka wa hatua za kuwachukulia madiwani hao wanaodaiwa kusaliti chama kwa kuungana na wapinzani.
Wakati CCM wakimlinda meya wao, madiwani hao waliibua tuhuma nyingine nzito kwa vigogo wa chama na serikali mkoa kuwa walitumika kuwarubuni kwa rushwa ili waondoe hoja yao.
 
Wakizungumza na gazeti hili jana, madiwani hao walisema kuwa kikao cha NEC wiki iliyopita kilimalizika bila kuwachukulia hatua yoyote, lakini wakashangazwa na uamuzi wa katibu wa chama Mkoa wa Kagera.
“Huyu Katibu Revelend Mushi alijipachika jukumu la kutuandikia barua za onyo zinazotutaka tusitende kosa lolote ndani ya kipindi cha miezi sita.
“Lakini tunahoji ni kwanini yeye, Mwenyekiti wake, Costnacia Mliye na Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe wamekuwa mstari wa mbele kumtetea meya. Sisi tunawaonyesha ufisadi wake wao wanamkumbatia,” alisema mmoja wa madiwano hao.
Waliongeza kuwa Rais Kikwete alitambua hoja yao na kuamuru viwanja vigawiwe upya kwa walengwa na ujenzi wa soko la kisasa ufuate utaratibu, lakini wakahoji kwanini chama kinageuza lengo na kutaka kuwafukuza.
“Hivi hii itakuwa CCM ya wapi inayokubali kupoteza madiwani wanane kwa lengo la kumlinda mtu mmoja (meya) asiondolewe? Maana hata Amani akiondolewa leo lazima kiti kitarudi kwetu,” alisema diwani mwingine.
Madiwani hao walikwenda mbali zaidi wakifichua ufisadi uliofanywa na viongozi wa chama ili kufanikisha vikao vya kuwafukuza uanachama.
Walisema kuwa mikutano yote ya chama hufanyika katika ukumbi wa ofisi zao, lakini wakahoji zilikotoka fedha za kulipia vikao vyote hivyo vilivyofanyika katika hoteli ya kitalii ya Walk Guard pamoja na kulipia posho za wajumbe.
Kwa mujibu wa mmoja wa wajumbe waliohudhuria vikao hivyo, gharama ya ukumbi uliotumika kwa siku ni sh 150,000 na kwamba kila mjumbe alilipwa posho ya sh 30,000.
Madiwani hao walidai kuwa fedha hizo ni za kifisadi kwani zilichangishwa kwa nguvu kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na makampuni ya ujenzi waliokuwa wapewe zabuni za ujenzi, wakitishwa kuwa meya aking’oka na wao pia kazi imekwisha.
“Hizi fedha zilikusanywa na mfanyabiashara mmoja (wanamtaja). Kwa siku mbili. Zilikuwa zinatembezwa sh milioni 40 kwetu na viongozi wa CCM ili kutununua tuachane na hoja yetu.
 
“Sisi tulishasema hatukatai miradi hiyo isipokuwa hatumtaki meya aitekeleze kwa kuwa si muadilifu, aondoke tuchague mtu muadilifu na muwazi. Amani mwenyewe alishinda kwa rushwa sasa amegeukwa,” alisema mmoja wa madiwani hao.
Waliongeza kuwa katika kutafuta huruma ya wananchi, meya Amani amegeuza mgogoro huo kuwa wa udini akidai kwamba madiwani Waislamu ndio wanampinga kwa sababu ni Mkristo.
Hivi karibuni, madiwani hao walimgeuka Rais Kikwete, wakipinga uamuzi wake wa kumtaka meya kumaliza tofauti zake na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwa kile walichodai mgogoro huo si ugomvi kati ya wawili hao.
Madiwani hao walipinga kauli hiyo wakisema suluhu ni kupinga ufisadi wa meya, kwani hakuna ugomvi binafsi kati yake na mbunge.
Akihutubia mkutano mjini Bukoba, Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo lazima uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano “yasiyokuwa na msingi”.
Madiwani hao 15 walisema malumbano yaliyopo ni ya msingi kwa kuwa watu watakaobebeshwa deni la kurejesha mikopo inayochukuliwa na meya ni wakazi wa Bukoba, si meya mwenyewe.
Walisema rais ameonekana hafahamu kiini cha mgogoro, kwani kinachopingwa si miradi, bali utaratibu ambao meya ametumia kuanzisha miradi hiyo kifisadi bila kuzingatia maslahi ya wananchi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Kwa mujibu wa kanuni za manispaa hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM, ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.
Hata hivyo katika orodha hiyo, waliamua kumwondoa Balozi Kagasheki kwa vile ni waziri na sehemu ya serikali.
Hata hivyo, inajulikana kuwa hata Kagasheki anawaunga mkono ingefikia hatua ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.

Tuesday, August 13, 2013

Baadhi ya wanafunzi waliosaidiwa na Mfuko wa Elimu Mbeya (MBEYA Education TRUST Fund)


Baadhi ya wanafunzi wanaolipiwa ada na vifaa vingine vya shule na mfuko wa elimu mbeya walipofika ofisi za mfuko huo Mbeya (mfuko wa elimu mbeya ulioanzishwa na Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi kwa nia ya kusaidia wanafunzi wanaotoka familia zenye uwezo mdogo kiuchumi jijini mbeya)

KUTOKA FACEBOOK: Wilfred Rwakatare ameandika kutoka India anakopatiwa matibabu....

Habari waheshimiwa wananchi,poleni sana kwa majukumu ya kulijenga taifa.
Nikiwa ugenini India,napata mshituko na taarifa za kusikitisha kutoka huko nyumbani hasa juu ya rafiki yangu Sheikh Issa Ponda na wageni waliobahatika kuikanyaga ardhi ya Zanzibar.
kuna nini? manahodha wako wapi?
Salamu zangu za pole kwa swahiba wangu, ‘mjukuu wangu’ Sheikh Issa Ponda. namtakia uponyaji wa haraka na kila lenye kheri,naungana naye kwa sala. Pia niwape pole ndugu na watanzania wote waliozipokea habari hizi na kushika tama.
Nichukue fursa hii kukuhimiza wewe mheshimiwa,kutokuchoka kuliombea taifa letu la Tanzania, tunaziona dalili zote za kuipata Tanzania tuitakayo hivi karibuni.

Mh. Joseph Mbilinyi "SUGU" akiongea na wananchi wa Mbalizi Mbeya hivi karibuni


Kikao cha Kamati ya Bunge ya Uzazi Salama na WRA

Thanks for encouraging words Wurie Bah Mothers and babies will survive if ALL participate to make a difference. EVERYONE!
Mhe. Joseph Mbilinyi akichangia hoja kwa ajili ya uhai wa akinamama na watoto wachanga

Monday, August 12, 2013

SHIRIKI KUJADILI NA TUMA MAONI YA RASIMU, MABARAZA YA CHADEMA KATIBA MPYA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo kinaanza rasmi kuendesha Mabaraza ya Katiba, ambapo wananchi wote watashirikishwa kujadili na kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba Mpya, kwa njia mbalimbali kama ifuatavyo;

1. Mikutano ya hadhara, itakayoanza leo katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiongozwa na 
    timu mbili za viongozi wakuu, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dkt. 
    Willibroad Slaa. 
    
    Mikutano hiyo itafanyika nchi nzima. Ratiba ya mikutano yote, itatolewa kwa umma, 
    kupitia vyombo vya habari (mainstream & social media).

2. Kutuma ujumbe mfupi kwa simu. Mwananchi anaweza kutuma maoni yake ya Katiba 
    Mpya kupitia simu ya mkononi, kwenye NAMBA HII YA SIMU; 0789 24 82 24.


4. Mitandao ya kijamii, mf; Jamii Forums, facebooks, twitter, group emails, k.m mabadiliko, 
    wanabidii n.k, utaratibu wake utatolewa kwa umma, kupitia vyombo vya habari, ikiwa ni 
     pamoja na kuwekwa hapa, namna ambavyo Watanzania wote watashiriki kutoa maoni 
     yao kwa njia hii.




Tumaini Makene
CHADEMA Senior Information(Press) Officer
0752 691569/ 0688 595831

CHADEMA inamuondoa Kaburu Mweusi nchini? Iungwe Mkono!

na Bryceson Mathias
CHAMA cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, hivi karibuni kimewahakikishia watanzania kuwa kitafanya kila linalowezekana kurejesha mali zote za Taifa zilizouzwa kinyemela kwa mikataba mibovu.
Ni rai yangu, Kama wenye mapenzi mema na nchi hii wanaona viongozi na CHADEMA inafanya kazi ya kumuondoa Kaburu Mweusi nchini, ili watoto wetu, vijukuu, vitukuu waje kuwa na rasilimali endelevu, basi wapongezwe na kuungwa mkono.
Mbowe alidai kuwa, Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wenzake walipigana kuwaondoa Makaburu weupe na hivyo CHADEMA nao sasa wanafanya kazi ngumu ya kumuondoa Kaburu weusi ili watoto wanaokuja waweze kufaidi rasilimali zilizopo nchini.
Mbowe alisema hayo akitembelea Kata za jimbo la Hai, akiwa na wabunge zaidi ya 11 wa Chadema toka majimbo mbalimbali na kuweka wazi kuwa, ili kufanikiwa vita hivyo, watahakikisha Katiba mpya inaweka wazi ulazima wa kuanika mikataba yote ya kiuchumi iliyoingiwa na serikali.
Kauli ya Mbowe, imepokewa kama kufutwa machozi ya wananchi wengi wanaopenda haki zao zilizopiganiwa na Nyerere zirejeshwe, wakifananisha na Wana Ndoa waliofiwa watoto, hivyo mke kuwa na Ujauzito wenye Uhakikika wa mtoto atakayeishi ni furaha kwao.
Mwenyekiti huyo ambaye ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni,  alitolea mfano wa shamba alilopewa mwekezaji anayezalisha sukari la TPC, akisema hakuna anayejua ni kiasi gani cha fedha kinachoingia serikalini wala kilichoandikwa kwenye mkataba huo.
Mbowe alidai Mwekezaji huyo alipatiwa eneo kubwa la shamba pamoja na maji, huku wananchi wa maeneo hayo wakitaabika kwa uhaba wa ardhi.
“Hatuwezi kuangalia mali yetu ikienda na wananchi wanataabika. Tukipata katiba mpya lazima mali zote zilizochukuliwa na wawekezaji mikataba irudiwe na iwekwe hadharani.
“Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na viwanda vingi vilivyokuwa vinafanya kazi vizuri, lakini wamepewa wawekezaji ambao kwa sasa hakuna anayejua mkataba walioingia na serikali na viwanda vingi Moshi vimekufa,” alisema.Mbowe.
 
Mbowe aliwakumbusha watanzania Juhudi za Mwalimu Nyerere na kusema, Nyerere na  viongozi wenzake walipigana kuwaondoa Makaburu weupe na hivyo kuwa CHADEMA sasa nayo inafanya kazi ngumu kumuondoa Kaburu mweusi ili watoto wanaokuja waweze kufaidi rasilimali zilizopo nchini.
 
“Hivyo wananchi wangu wa Hai mkiniona niko kimya natafuta ukombozi wa nchi hii, baada ya kutoka hapa nitafanya mikutano nchi nzima, lakini ninawaahidi tukimaliza Bunge la Katiba lazima nije kushinda na nyie kusikiliza zaidi kero zenu,” alisema Mbowe.
 
Angalizo la Mbowe na Chama chake cha Chadema, litufumbuwe macho watanzania, kwa sababu ni ukweli usiopingika kwamba, viwanda vyote vya sukari nchi kikiwemo Mtibwa, Kilombero na Kagera, sasa hivi vimekuwa havina faida kwa wananchi na wafanyakazi wa  maeneo husika.
 
Yapo maeneo mengi ya uwekezaji, ambayo yana tatizo la mikataba mibovu inayodaiwa ni ya siri, ambayo licha wananchi kukosa maeneo ya kulima, lakini wanakosa hata haki za kupata maendeleo yao wenyewe kuhusiana na kuwepo kwa uwekezaji huo.
 
Pengine kwa tamko la CHADEMA na viongozi wake, limegusa mioyo ya watanzania, ambao kwa hapa nchini katika uwekezaji, wamekuwa watumwa wa wawekezaji katika nchi yao wenyewe, huku wakifanyizwa kazi utumwa kwa kipato duni, ndani ya rasilimali walizoziasisi wenyewe, huku faida ya kutisha ikisombwa na kusafirishwa kwenda nje.

Mbowe, Slaa wapeleka rasimu kwa ‘chopa’


MWENYEKITI na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wanaanza rasmi ziara nchi nzima kwa kutumia helikopta kwa ajili ya kuzindua mabaraza ya Katiba ya chama.
Ziara hizo zitakazowashirikisha wabunge wote na viongozi wengine zinaanza rasmi leo, ambapo mwenyekiti Freeman Mbowe atazindua mpango huo mkoani Mara.
Wakati Mbowe akianzia mkoani Mara, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa atakuwa mkoani Tanga kuanzia Agosti 15 na kuendekea katika mikoa mingine.
Taarifa kutoka ndani ya CHADEMA zinasema kuwa viongozi hao watapita katika kila jimbo la uchaguzi ambapo kila mkoa watakaa siku zisizopungua nne wakijadili rasimu hiyo ya Katiba na wafuasi wao.
Kutoka mkoani Mara, mwandishi wetu anaripoti kuwa wakazi wa Tarime wamemwandalia mapokezi makubwa Mbowe ambaye atawasili wilayani humo kesho alasiri akitokea Serengeti.
Mwenyekiti wa madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Charles Mbusiro, aliliambia gazeti hili kuwa wamejiandaa vyema kumpokea kiongozi huyo.
Alisema kuwa Mbowe na timu yake watazungumzia juu ya mchakato wa Katiba mpya unaoendelea kwenye rasimu pamoja na hati iliyozuiliwa kwa ajili ya kuzinduliwa halmashauri ya mji wa Tarime iliyoanza kufanya kazi Julai mosi mwaka huu.
Aliongeza kuwa Mbowe atafuatana na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu, Prof. Abdallah Safari na viongozi wengine.
Wakati Mbowe akianza mashambulizi hayo kanda ya Ziwa, Dk. Slaa na viongozi wengine wataanzia Kanda ya Kaskazini kwenye mkoa wa Tanga.
Kwa mujibu wa Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje, Dk.Slaa atafanya mikutano ya hadhara katika wilaya zote za mkoa huo akizungumzia rasimu ya Katiba mpya.
Kama itakavyokuwa kwa Mbowe, pia Dk. Slaa naye atatumia usafiri wa helikopta katika kuzitembelea wilaya hizo za Lushoto, Handeni, Korogwe, Muheza na Tanga mjini.
Bahweje alisema kuwa chama hicho ngazi ya mkoa kinaendelea na mikutano ya hadhara na ya ndani kwa lengo la kuelezea mkakati wake.
Katika hatua nyingine, Mbowe amesema hana mpango wa kuliacha jimbo lake la Hai kwa ajili ya kwenda kugombea ubunge Moshi Mjini kama anavyozushiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mbowe alitoa kauli hiyo baada ya kukuwepo na taarifa kuwa katika uchaguzi ujao atagombea ubunge Moshi mjini, jimbo ambalo kwa sasa linaongozwa na Philemon Ndesamburo (CHADEMA).
Akizungumza na wananchi wa kata ya Hai mjini juzi, Mbowe alisema hana mpango wa kuliacha jimbo hilo na kwamba uvumi unaosambazwa ni kuwatia hofu wananchi.
“Wananchi wa Hai nimepata taarifa kuwa kuna maneno yanaenezwa na CCM kwamba nina mpango wa kuwaacha wananchi wangu na kwenda kugombea Moshi mjini au Dar es Salaam, naomba niseme kuwa taarifa hizo si sahihi nitaendelea kuwatumikia hadi mtakapoamua nyie.”
“Nimetembea na wabunge wenzangu kwenye kata mbalimbali za jimbo langu, tumesikiliza kero zenu lakini wabunge wamefurahishwa na jinsi wananchi wangu wanavyoniita kaka na mimi nawaambia CCM hili ni jimbo la kaka,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbowe alitangaza vita na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga, pamoja na Katibu wa CCM wilaya, Hassan Mtenga, kwa kile alichoeleza kuwa ni kwa kufanya siasa zisizo za kistaarabu.
Mbowe alizungumzia suala la uwanja wa Sabasaba uliokuwa ukimilikiwa na halmashauri kutaifishwa na kuzuia mikutano ya upinzani isifanyike hapo.
“Hatuwezi kuwa watumwa ndani ya nchi yetu, uwanja wanaoita wa CCM ulikuwa ni wa halmashauri na ni wa Watanzania wote hakuna haja ya kuukumbatia uwanja huo na sisi kufanyia mikutano standi,” alisema.

CHADEMA: Tutarejesha mali zilizoporwa


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa kitapigana hadi tone la mwisho la damu kurejesha mali zote za wananchi zilizouzwa kinyemela.
Mbowe akiwa katika ziara yake kutembelea kata zote za jimbo la Hai, akiambatana na wabunge zaidi ya 11 wa chama hicho kutoka majimbo mbalimbali, alisema ili kufanikiwa katika vita hivyo, watahakikisha katiba mpya inaweka wazi ulazima wa kuanika mikataba yote ya kiuchumi iliyoingiwa na serikali.
Mwenyekiti huyo ambaye ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni alitolea mfano shamba alilopewa mwekezaji anayezalisha sukari la TPC, akisema hakuna anayejua ni kiasi gani cha fedha kinachoingia serikalini wala kilichoandikwa kwenye mkataba huo, ambao umempatia mwekezaji huyo eneo kubwa la shamba pamoja na maji huku wananchi wakitaabika kwa uhaba wa ardhi.
“Hatuwezi kuangalia mali yetu ikienda na wananchi wanataabika tukipata katiba mpya lazima mali zote zilizochukuliwa na wawekezaji mikataba irudiwe na iweke hadharani.
“Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na viwanda vingi vilivyokuwa vinafanya kazi vizuri, lakini wamepewa wawekezaji kwa sasa hakuna anayejua mkataba walioingia na serikali na viwanda vingi Moshi vimekufa,” alisema.
Alisema Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wenzake walipigana kuwaondoa Makaburu weupe na hivyo CHADEMA nao wanafanya kazi ngumu kumuondoa Kaburu weusi ili watoto wanaokuja waweze kufaidi rasilimali zilizopo nchini.
“Hivyo wananchi wangu wa Hai mkuniona niko kimya natafuta ukombozi wa nchi hii baada ya kutoka hapa nitafanya mikutano nchi nzima, lakini ninawaahidi tukimaliza Bunge la Katiba lazima nije kushinda na nyie kusikiliza zaidi kero zanu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema katiba ya sasa imetumiwa vibaya na viongozi walioko madarakani kuwalimbikizia wananchi kesi pamoja na kutowachukulia hatua viongozi wanaoiba rasilimali za umma.
Alisema wafungwa wengi magerezani ni wale wezi wadogo wadogo huku viongozi walioiba mabilioni wakiendelea kufurahia maisha uraiani.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, alisema kuwa kama kuna kiongozi wa upinzani ambaye akifa CCM watafanya sherehe ni pamoja na Mbunge wa Hai Freeman Mbowe.
Alisema Mbowe amekuwa akifanya kazi ngumu na kuleta mafanikio makubwa yakiwemo ya kuwa na wabunge wengi vijana ikiwemo yeye.
Miongoni mwa wabunge walio kwenye ziara hiyo ni pamoja na Ezeckiel Wenje, Peter Msigwa, Joshua Nasari, Lucy Owenye, Grace Kiwelu, Joseph Selasini, pamoja na madiwani wa CHADEMA kutoka Moshi, manispaa na Hai.
Wakati huo huo CHADEMA imepinga kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba kwamba hawatapokea maoni yatayopelekwa kwa njia ya Chopa.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Mabibo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema chama chao kitatumia kila njia kuwafikia Watanzania na kuwaelewesha rasimu ya Katiba mpya na msimamo wao.
Mnyika alisema kila chama cha siasa sasa kinawafikia wananchi wake, kuwaelewesha na kupata maoni yao kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya, hivyo haoni kama ni kosa kwao.
Alisema CHADEMA imeshaanza ziara na kueleza kwamba mwenyekiti wao Freeman Mbowe akishirikiana na Tundu Lissu wako mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kati huku Dk. Willibrod Slaa na Mabere Marando wakitoa elimu mikoa ya kusini na kaskazini.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo alisema wakiwa katika mchakato huo, Jaji Warioba akishirikiana na wenzake ametaka kupindisha sheria ili wampe madaraka Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa wajumbe wengine zaidi ya 100 kuingia katika Bunge la Katiba jambo ambalo CHADEMA haikubaliani nalo.
Alisema kutokana na hilo pamoja na mengine ambayo yanaweza kuchomekwa, wamemwagiza Lissu kukatiza ziara yake ili ashirikiane na wanasheria wengine kukabilina na jambo hilo.



“Baada ya kutokea dharura hiyo, nawaomba wananchi wangu nikachukue nafasi ya Lissu … nitaondoka Jumapili, nitakaa huko kwa siku 12 ili niweze kusaidiana na mwenyekiti wangu kupata maoni ya Watanzania,” alisema.
Mnyika alisema pamoja na hilo, CHADEMA imetengeneza kitabu kinachozungumzia msimamo wao kuhusu muundo wa Katiba mpya ambacho wameanza kukisambanza kwa wananchi kwa gharama ya sh 300.
Kiongozi huyo aliwataka Watanzania na Wanachadema ambao wanapenda mabadiliko kukinunua kwa ajili ya kupata uelewa kuhusu rasimu hiyo na nini wanapaswa kuchangia.
Wakati huohuo, Mnyika aliwataka wananchi na Wanachadema kumchagua mgombea uenyekiti wa mtaa wa Sahara Relini Mayunga Kadwisha katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho Agosti 11, mwaka huu.
Akimnadi mgombea huyo, Mnyika alisema nchi hii inapaswa kuongozwa na mtu anayependa mabadiliko hasa CHADEMA na si vinginevyo.
‘Wananchi wa Sahara na Reline, mchagueni Kadwisha siku ya Jumapili kwa ajili ya maendeleo ya mtaa wenu … hakuna mgombea mwingine, na hapa nafikiri kama CHADEMA isingemweka mgombea huyu likawepo jiwe, mngechagua jiwe kuliko CCM,” alisema Mnyika.

Tuesday, August 6, 2013

KAULI JUU YA KUONDOKA TENDWA, KUINGIA JAJI MUTUNGI, MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA


John Tendwa alipaswa kuwa ameondoka kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, tangu mwaka 2008, alipofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Aliendelea kufanya kazi zake hata baada ya muda wa mkataba wake alioongezewa kuwa umefikia mwisho, hivyo alikuwa anakalia ofisi hiyo ya umma, kinyume cha sheria.
Ametumia muda huo wa miezi kadhaa, aliokuwa anakalia ofisi ya umma kinyume cha sheria, kuropoka na kuharibu demokrasia, kwa manufaa ya mamlaka iliyomteua na CCM. Kutokana na mwenendo (maneno na matendo) wake mbovu, CHADEMA ilitangaza kutokumpatia ushirikiano wowote, yeye kama Tendwa. Ikamtangaza kuwa adui wa demokrasia nchini.

Kwa muda wote huo, CHADEMA ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Badala ya kuifuta CHADEMA na kufanikisha dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye.

Kuondoka kwa Tendwa hakuzuii  kutekelezwa kwa mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, iliyomkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa, hivyo akasababisha kutokea kwa mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Nyololo, Iringa.

Hivyo CHADEMA, kupitia Kurugenzi ya Habari na Uenezi, inataka kauli ya Rais Jakaya Kikwete juu ya utekelezaji  wa mapendekezo hayo kwa Tendwa watu wengine, akiwemo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na wote waliotajwa katika ripoti hiyo ya chombo cha serikali, kuwa walivunja sheria za nchi na kusababisha mauaji ya mwandishi, raia asiyekuwa na hatia.

Tunamkaribisha 'with benefit of doubt', msajili mpya, Jaji  Francis Mutungi, kwenye kazi na majukumu yake mapya. Wapenda demokrasia na maendeleo nchini, wanamtarajia atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia haki, sheria na utawala bora, asije akapita njia ya Tendwa.

Kupitia mchakato wa Katiba Mpya unaojadiliwa sasa hivi, CHADEMA tunapendekeza Ofisi ya Msajili ipewe uhuru zaidi na uteuzi wake, usiwe suala la Rais kuamka tu na kuamua kuteua bila wahusika kuomba, kuchujwa na kuthibitishwa na mamlaka nyingine tofauti na iliyoteua.

Tunatambua kuwa msajili mpya aliwahi kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani, kwa muda mfupi, kisha akateuliwa kuwa Jaji na akateuliwa pia nafasi zingine. Na sasa mwaka mmoja baada ya kutumikia nafasi hizo, ameteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa. 

Jaji Mutungi, anapaswa kuonesha kwa maneno na vitendo kwamba hatakuwa kama Tendwa, kwa kuanza kushughulikia matendo ya kiharamia yaliyofanywa na Green Guards wa CCM kwenye chaguzi za madiwani, zilizomalizika karibuni, ambazo si tu yalikuwa kinyume na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambayo Jeshi la Polisi wanatakiwa kuchukua hatua, bali pia yalikuwa kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa. Hivyo yako kwenye mamlaka yake.

Jaji Mutungi, amshauri Rais Jakaya Kikwete kushughulikia mapendekezo ya Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, juu ya uvunjifu wa sheria wa wazi uliofanywa na askari polisi na John Tendwa, hivyo kusababisha mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012, huko Nyololo, Iringa.

Aidha, Jaji Mutungi anapaswa kumshauri Rais Kikwete kujibu na kufanyia kazi barua mbili alizoandikiwa na CHADEMA juu ya kuunda Tume Huru ya Kimahakama/Kijaji, kuchunguza mauaji yaliyofanyika kwenye shughuli halali za kisiasa za CHADEMA.

Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mauaji mfululizo mkoani Morogoro na Iringa, CHADEMA ilimwandikia barua Rais Kikwete kumtaka aunde Tume ya Kimahakama kuchunguza utata wa vifo hivyo na vingine kadhaa vilivyotokea kwenye shughuli halali za kisiasa, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ili ukweli ujulikane, haki itendeke na wahusika wachukuliwe hatua, hadi sasa rais hajafanya hivyo.

Itakumbukwa pia kuwa baada ya mlipuko wa bomu la Arusha, kwenye mkutano wa kampeni, CHADEMA pia ilimtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake kuunda Tume Huru ya Kimahakama, ili ushahidi juu ya tukio hilo uwasilishwe, hadi sasa pia rais yuko kimya. Hivyo kwa nafasi yake, msajili mpya atoe ushauri kwa rais kuchukua hatua hizo, ili vyama vitimize wajibu wa kikatiba kufanya kazi zake kwa haki, uhuru na sheria za nchi zinazosimamia shughuli za vyama vya siasa nchini.

Imetolewa leo na;
 
Tumaini Makene

Tendwa: Kwa heri, ila umedumaza Demokrasia


 
WAKATI aliyekuwa msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa alikuwa akikabiliwa na Hamu ya kukifuta Chama cha Siasa cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye ulingo huo, hamu hiyo imedhihirishwa na usemi wa mkamia maji hayanywi na akinywa hutapika.
 
Kabla Tendwa hajakifuta Chadema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Mheshimiwa Jaji Francis S.K.Mutungi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, hivyo tarajio na makusudi ya Tendwa dhidi ya Chademea, yameyoyoma gizani.
 
Taarifa iliyotolewa Dar Es Salaam, Jumatatu, Agosti 5, 2013, na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza Ijumaa iliyopita Agosti 2, 2013.

 
Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Tendwa ambaye amestaafu Utumishi wa Umma kwa mujibu wa sheria, akieelezwa na wadau wa Siasa na hasa wapinzani na Wapenda haki kuwa alikuwa kikwazo cha Demokrasia nchini.
Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, hivyo kuteuliwa kwake kumeelezwa na washiriki wana siasa kusipelekee yale aliyoyafanya Tendwa na kusababisha sintofahamu ya vurugu za Kidemokrasia.
 
Tumezoea kusikia mtu anapostaafu watu humzungumza kwa mazuri, lakini cha kusikitisha jamii kwa ujumla wake imekuwa na mtazamo hasi kutokana na wajibu wa Tendwa alipokuwa kwenye majukumu yake ya usajili wa vyama vya siasa.
 
Pengine niseme matatizo si changamoto aliyokuwa nayo Tendwa, sipendi yawepo kwa Jaji Mutungi, na tutakuwa na Imani hiyo kwa sababu kimsingi Mutungi wakati mwenzie akiwa katika wadhifa huo, alipata nafasi ya kusikia akilalamikiwa kwa mambo kadhaa, ayaepuke.
 
Ingawa muda wa Utumishi wa Tendwa ulikuwa umekwisha, lakini akapata bahati ya kuongezewa muda huo kwa msingi pengine alikuwa mtendaji mzuri wa kazi hivyo, utumishi ulikuwa bado unahitaji. Kilichodhaniwa na wengi sicho kilichojiri kwa wanasiasa na jamii.
 
Kiujumla nyakati hizi za mwishoni, Ofisi ya Msajili ikiongozwa na Tendwa ilikuwa na Kauli za Vitisho na Ubabe uliokuwa unakiuka Sheria kadhaa za Demokrasia ya Vyama Vingi, kiasi wadau wake walikuwa hawaamini iwapo ofisi hiyo ndiyo yenye watu wenye upeo wa Sheria.
 
Kwa kuwa wapenda Demokrasia na Maendeleo nchini wanamtarajia Jaji Mutungi atomize wajibu wake kwa kuzingatia haki, sheria na utawala bora, basi asije akapitia njia za Tendwa  
Ila anapaswa kuonesha kwa maneno na vitendo.
 
Aidha tunamtaka Jaji Mutungi aanze na kushughulikia matendo ya kiharamia ambayo yamekuwa yakifanywa kwenye chaguzi kubwa na ndogo, yaliyosababisha watu kupoteza maisha na ulemavu wa kudumu kwa wananchi na wanasiasa wote.
 
Hata hivyo Jaji pia anatakiwa kutoa Ushauri kwa Serikali na Jeshi la Polisi kuacha kutumia nguvu za ziada na Utawala Bora, juu ya uvunjifu wa sheria wa wazi uliokwisha fanywa na askari polisi dhidi ya vifo na kuumizwa kwa wandishi na wananchi, pasipo kosa lolote
 
Na Bryceson Mathias

Wiki ngumu kwa CCM: MEYA WAO ANG’OLEWA BUKOBA


IMEKUWA wiki ngumu kisiasa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho viongozi wake wa kitaifa wanahaha kila kona kujaribu kunusuru mgawanyiko uliopo.
Mambo matatu makuu yanayokiandama chama hicho ni mgogoro wa meya wao na madiwani mjini Bukoba, uchaguzi wa wenyeviti wa halmashauri mkoani Kigoma na kukwama kwa propanda zao za ugaidi dhidi ya CHADEMA.
Madiwani wa CCM, CHADEMA na CUF, tayari juzi walimfukuza rasmi Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
Waliopiga kura ya kutokuwa na imani na meya ni madiwani 15 waliosaini fomu ya hati ya kumtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuitisha kikao cha dharura kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.
 
Diwani wa 16 ambaye hakusaini lakini aliridhia uamuzi huo ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki, ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii.
Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa madiwani hao kufikia uamuzi huo, kwani walikumbana na mikikimikiki ya meya mwenyewe akisaidiana na uongozi wa CCM mkoani na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe.
Habari kutoka vyanzo vya karibu na uongozi wa CCM mkoani Kagera vililiambia gazeti hili kuwa kutokana na uamuzi huo, na kwa kuwa CCM na serikali mkoani humo hawataki meya aondoke, chama hicho tawala kimepanga kuwafukuza madiwani wao walioweka sahihi zao kumfukuza meya.
Tayari taarifa zimevuja kwamba CCM itaitisha kikao Agosti 10, mwaka huu kuwafukuza madiwani wake hao ambao wameapa kwamba liwalo na liwe, hawawezi kuacha ufisadi utumike kama kigezo cha kuleta miradi Bukoba.
Baadhi ya madiwani waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa wanatembea na kadi zao za CCM mfukoni tayari kuzikabidhi iwapo uongozi utaamua kulinda ufisadi wa meya na kuwachukulia hatua wao.
Vyanzo vyetu vya habari vinasema hatua ya madiwani hao kumwondoa meya ilikuwa kama igizo. Mkurugenzi alikataa kuitisha kikao cha baraza la madiwani ambacho ndicho kingemfukuza.
Lakini kwa kutambua kuwa idadi iliyohitajika ili meya aondoke ni madiwani 16 na tayari ilikidhi matakwa hayo, madiwani hao walikusanyika kufanya uamuzi huo mgumu.
Kabla ya hatua hiyo kufikiwa, juzi asubuhi meya na mkurugenzi wa manisapaa hiyo walikwenda mahakamani kuweka pingamizi la kuzuia madiwani kuitisha kikao cha kumwondoa meya, kwa hoja kwamba shauri lao lilikuwa mahakamani.
Hata hivyo, meya na mkurugenzi waligonga kisiki mahakamani, baada ya kuambiwa kuwa shauri lililokuwa mahakamani lilikuwa tofauti na uamuzi waliokuwa wanataka kuchukua.
Taarifa hizo zilisema kuwa uamuzi wa meya na mkurugenzi kwenda mahakamani ulitokana na agizo la mkuu wa mkoa ambaye alimwandikia mkurugenzi huyo akimzuia kuitisha kikao cha baraza la madiwani kama alivyokuwa ametakiwa na madiwani hao kwa mujibu wa kanuni.
Baada ya madiwani hao kuona jitihada za meya na mkurugenzi kuzuia azima yao, na walipogundua mahakama imekataa kutoa hati ya zuio la kikao chao, walikusanyika katika ofisi za manispaa hiyo ili kufanya kikao, lakini mkurugenzi alikataa kufungua.
Badala yake waliamua kufanya kikao nje ya ukumbi wa halmashauri, wakamfukuza meya na kuandika muhtasari ambao wataupeleka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Taarifa zaidi zinasema kabla ya hatua hiyo ya madiwani, CCM ilikuwa imeitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kujadili hatima ya sakata hili, hasa madiwani wa chama chao.
Uamuzi wa kuita kikao hicho ulitokana na maagizo ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Phillip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, ambao kwa nyakati tofauti Jumamosi iliyopita waliwasiliana na Mkuu wa Mkoa na Mweyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera kuwataka wamalize mgogoro huo “kwa busara.”
Katika kikao hicho cha Jumapili, mara baada ya ufunguzi, wajumbe walikaa kimya kama walioduwaa. Ndipo alipoibuka mjumbe kutoka Karagwe na kutoa hoja kwamba madiwani wa CCM wafukuzwe kwa sababu wanachafua chama.
Hoja yake iliungwa mkono na wajumbekutoka Muleba na Missenyi. Hata hivyo, mkuu wa mkoa alionya kwamba hatua ya kufukuza madiwani hao ingepingana na ushauri aliopewa na Kinana na Mangula, wa kumaliza mgogoro kwa “kutumia busara.”
Akapendekeza kwamba wapewe siku saba za “kujirudi,” waondoe barua yao ya kutokuwa na imani na meya; na kwamba baada ya hapo kama watakataa ndipo wafukuzwe.
Inadaiwa kuwa mjumbe mwingine akasema kuwa hata ushauri wa mkuu wa mkoa una dosari, kwa kuwa madiwani hao walikuwa wameshaandika barua kwa mujibu wa kanuni, na zilikuwa zimepita siku nne, huku wakihesabu.
Kwa mujibu wa kanuni za halmashauri, barua kama hiyo ikishaandikwa, mkurugenzi analazimika kuita kikao ndani ya siku saba baada ya kumpa meya taarifa hizo ili ajiandae kujibu tuhuma zinazomkabili.
Mjumbe huyo alimuonya mkuu wa mkoa kwamba halmashauri haiongozwi na amri au maelekezo ya mkuu wa mkoa bali kanuni za halmashauri.
Kikao hicho cha Jumapili kiliahirishwa kwa mkanganyiko huo juu ya hatua wanayopaswa kuchukuliwa madiwani hao.

Friday, August 2, 2013

Mbeya Yetu: MBEYA BADO HAWAKOMI NA MAJANGA YA MOTO: BAADA ...

Mbeya Yetu: MBEYA BADO HAWAKOMI NA MAJANGA YA MOTO: BAADA ...:  Lori lenye namba za usajili  T97 AJL lenye tela namba T746 BKF lilipo acha njia na kupinduka na kuziba njia Lori  likishindwa kupi...