MUASISI wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edwin Mtei, amesema kauli ya
Kingunge Ngombale - Mwiru kwamba wazee wanaounga mkono muundo wa muungano
wa serikali tatu wamechanganyikiwa ni ya kutokujua hesabu.
Wakati Mtei
akijibu mapigo hayo, mkongwe mwingine wa siasa nchini, Jaji mstaafu Mark
Bomani, amesema kuwa anamvutia pumzi Kingunge hadi wiki ijayo.
Mwishoni mwa wiki
iliyopita, Kingunge alizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake
jijini Dar es Salaam na kuwashambulia wazee wenzake wanaounga mkono
mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya ya kuwa na muundo wa serikali tatu
kwamba ni sawa na watu waliochanganyikiwa.
Kingunge alifafanua
kuwa anashangaa kuona wanaopendekeza muundo huo miongoni mwao ni wazee
ambao walishiriki kuundwa kwa muungano uliopo mwaka 1964, ambao umeleta
mafanikio kwa kujenga udugu na umoja wa kitafa.
Alisema baadhi ya
viongozi wameshindwa kuthamini mafanikio ya muungano na hivi sasa mawazo
yao yote wamekuwa wakiyaelekeza kwenye vyeo vyenye marupurupu.
Akizungumza na
Tanzania Daima jana, Mtei ambaye pia ni Gavana mstaafu wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), alisema kuwa muundo wa sasa wa serikali mbili umeshindwa
kuondoa kero za wananchi, hivyo ili kuondoa malalamiko lazima kwenda kwenye
serikali tatu.
“Chama changu na
mimi mwenyewe tunataka serikali tatu. Sasa Kingunge kama anasema sisi
tumechanganyikiwa nadhani hajui hesabu hii nyepesi.
“Lazima tuwe na
serikali tatu; ya Tangayika, Zanzibar na ile ya Muungano. Muundo huu wa
serikali mbili ambao hata hivyo ni sawa na serikali moja ya Bara ambayo
imeimeza Zanzibar umeshindwa,” alisema.
Mtei alifafanua
kuwa chini ya muundo wa serikali mbili lawama na kero zimekuwa nyingi,
hivyo katika kuondosha kero hizo lazima serikali ziwe tatu na baada ya hapo
atakayetaka kujitenga aende afanye atakavyo bila kulazimishwa.
“Wengi wape, watu
wanataka serikali tatu, hivyo lazima twende huko. Na wala hatuendi
kupigania madaraka na vyeo kama anavyosema Kingunge, bali ni matakwa ya
watu,” alisema.
Naye Jaji Bomani
ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa uongozi wa
hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema kuwa kauli ya Kingunge ni nzito na
hategemei kama alinukuliwa vibaya.
“Naomba univumilie
nitazungumzia hilo pamoja na mambo mengine yanayopotoshwa wiki ijayo ili
kuyaweka sawa,” alisema.
Kingunge katika
mazungumzo yake hayo mbali na muundo wa serikali tatu pia alidai kuwa Chama
chake Cha Mapinduzi (CCM) kilikurupuka kuanza mchakato wa Katiba mpya
wakati haikuwa sera yao kwenye ilani ya 2010/2015.
Mkongwe huyo
amewahi kuwa mshauri wa masuala ya kisiasa wa Rais Kikwete katika awamu ya
kwanza ya utawala wake.
Alisema kuwa CCM
haikukaa pamoja kama walivyofanya kwenye mchakato wa kuingia kwenye mfumo
wa vyama vingi mwaka 1990.
Kauli yake hata
hivyo imetafsiriwa kama ya kupingana na uamuzi wa Rais Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa CCM, kwani licha ya suala hilo la Katiba mpya kutokuwamo
kwenye ilani ya uchaguzi, aliafikiana na hoja ya wapinzani akakubali
serikali yake ilifanyie kazi.
Kuhusu suala la
uraia wa nchi mbili, Kingunge alisema lilikuwa linasemwa pembeni lakini
sasa wanataka liingizwe kwenye Katiba.
“Mwanzo nilijua ni
utani, lakini nilishangaa suala hili kubwa kuliona limeingizwa kwenye
kijitabu kilichotolewa na chama changu na kupendekeza hivyo,” alisema.
Alisema suala la
uraia ni la nchi, hivyo chama kilipaswa kutoa nafasi kwa wananchi kujadili
kwa kina jambo hilo na si viongozi kujiamulia wenyewe.
Alisema amekuwa
kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kwa muda mrefu lakini hakuwahi
kusikia hata siku moja suala hilo likijadiliwa, jambo alilodai ni hatari.
|
No comments:
Post a Comment