KIONGOZI wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA) ameibana serikali ieleze
ni lini itaunda tume huru ya kuchunguza matukio yanayosababishwa na
mapambano kati ya askari na raia.
Mbowe alitoa kuali
hiyo wakati akiuliza swali la nyongeza bungeni akihoji kwa nini askari
wamekuwa wakienda na risasi na mabomu katika mikutano ya wananchi hasa ile
ya CHADEMA.
“Matukio ya
mapambano ya askari na raia sasa yameongezeka, hasa kwenye mikutano ya
CHADEMA, tumeiomba serikali iunde tume huru kuchunguza jambo hili, ni nini
kauli ya serikali kuhusu matukio hayo?” alihoji.
Akijibu maswali
hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Ame Silima, alisema
kuwa askari wanakabidhiwa silaha za aina mbalimbali wanapokwenda kwenye
mikusanyiko ya watu.
Silima alisema
matumizi ya silaha hutumika kuanzia ngazi za chini na hupanda kadiri vurugu
zinavyoongezeka.
Alisema polisi
hulazimika kutumia risasi kwa wafanya vurugu wazoefu.
Aliongeza kuwa
askari wamepata mafunzo ya kudhibiti vurugu na aina ya silaha zinazotumika
kwenye mikusanyiko ya watu.
Waziri Silima
alisema hali inapokuwa mbaya eneo la vurugu askari hulazimika kutumia silaha
kubwa zaidi kama watu hawataki kutawanyika.
Alibainisha kuwa
kwa kawaida jeshi hilo limekuwa likihimiza utii bila shuruti lakini
inaposhindikana matumizi ya nguvu hayaepukiki.
Kuhusu kuundwa kwa
tume huru, alisema mpaka sasa hakuna mahitaji hayo kwa kuwa jambo hilo
linafanywa na polisi.
Aliongeza kuwa
kama ukifika wakati tume hiyo itahitajika serikali haitasita kutekeleza
jambo hilo.
Awali katika swali
la msingi la Mbunge wa Jang’ombe, Hussein Mussa Mzee (CCM) alitaka kujua
kama mabomu ya machozi yana madhara kwa binadamu.
Alitaka pia kujua
kama polisi hawana mbinu au silaha nyingine wanazoweza kutumia ili kuepusha
madhara yanayotokea katika mikusanyiko ya watu.
Akijibu maswali
hayo, Silima alisema wananchi wanapaswa kujifunza kutii sheria bila shuruti
ili kuepusha mapambano na askari.
Alibainisha kuwa
mabomu ya machozi hayana madhara endelevu kwani silaha hizo zimefanyiwa
uchunguzi wa kimaabara na kukubalika kimataifa.
Alisema silaha
hizo zikitumiwa vizuri hazina madhara makubwa kwa binadamu zaidi ya kuwasha
macho na athari hizo hudumu kwa muda mfupi tu.
Silima alisema
kuna sheria za kitaifa na mikataba ya kimataifa inayoelezea matumizi ya
nguvu za polisi katika kudhibiti vurugu.
Alisema kulinga na
utendaji wa polisi na sheria hizo polisi hutumia silaha za aina nyingi
zikiwamo virungu, maji ya kuwasha, risasi baridi, mabomu ya machozi, mbwa
na farasi kwa kutegemea aina ya vurugu, wingi wa watu na aina ya silaha
walizonazo.
Mwisho
|
No comments:
Post a Comment