HUKU akijitapa kuwa ndiye mlinzi wa kanuni za Bunge, na akiwalaumu wabunge,
hasa wa upinzani, kwa kukiuka kanuni hizo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai,
amebainika kuwa alivunja kanuni nyingi za Bunge siku ilipozuka zogo bungeni.
Kwanza, alivunja kanuni inayomtaka ampe fursa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni kuzungumza.
Pili, alivunja kanuni inayomruhusu kumchukulia hatua mbunge aliyedharau kiti
cha spika.
Tatu, alivunja kanuni inayomtaka kuahirisha Bunge kabla ya kuruhusu askari
kuingia bungeni unapotokea mzozo.
Kanuni ya 5 (1) inasema: “Katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa katika
ibara ya 84 ya katiba, spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni
hazikutoa mwongozo basi spika atafanya kazi kwa kuzingatia katiba, sheria
nyingine za nchi kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa
mabunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge
unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.” Mbowe hakupewa fursa hiyo.
Kwa utamaduni wa mabunge ya Jumuiya ya Madola ambao unatumiwa na Bunge letu,
Mbowe ni sawa na Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.
Tofauti yao ni moja tu, kwamba waziri mkuu ana dola, na yeye hana.
Kwa kuzingatia utamaduni huo, viongozi hawa wanaposimama wakati wowote, kiti
cha spika kitamwomba mbunge anayezungumza aketi chini kisha mmoja kati yao
ambaye atakuwa alisimama atapewa nafasi ya kutoa hoja yake.
Kanuni ya 74 - (1) ndiyo ilipaswa kutumiwa na Ndugai kumshughulikia Mbowe
kama alidharau kiti, lakini pia hakuitumia.
Inasomeka: “Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka ya
spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge ikiwa: (a) kwa maneno au vitendo, mbunge huyo anaonyesha dharau kwa
mamlaka ya spika; au (b) mbunge huyo anafanya kitendo chochote cha makusudi cha
kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo.
Kama Ndugai angezingatia kanuni za kudumu zinazoliongoza Bunge ili kudhibiti
fujo kama hizo bungeni, alitakiwa kutumia kanuni ya 76 - (1) badala ya
kuwaingiza ukumbini watu wasiopaswa ili kuwadhalilisha baadhi ya wabunge wa
upinzani akiwemo kiongozi wao, Mbowe.
Kanuni hiyo inasema: “Kwa madhumuni ya kudhibiti fujo endapo ikitokea ndani
ya ukumbi wa Bunge na spika ataona kuna haja ya kutumia nguvu, basi anaweza
kuahirisha shughuli za Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa au kusitisha kikao kwa
muda atakaoutaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa na mpambe wa Bunge.”
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanautafsiri uamuzi wa Ndugai kama mbinu ovu
iliyokuwa imeandaliwa mapema ili kuwasonga wapinzani wasiweze kuujadili muswada
wa sheria wa kurekebisha sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013.
Ni wazi kuwa kasoro nyingi zilizopenyezwa katika muswada huo zisingeweza
kuafikiwa na wapinzani ili kuipa nafasi CCM kudhibiti mchakato wa katiba mpya
unaoendelea.
Katika vuta ni kuvute hiyo, wapinzani waliitaka serikali kuuondoa muswada huo
kisha kuufanyia marekebisho, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wakiwemo
Wazanzibari.
Serikali na kiti cha spika hawakuwa tayari kutekeleza masharti hayo, hatua
iliyoibua mvutano wa kikanuni hadi kufikia wabunge kupiga kura ya kuamua ama
mjadala uendelee au usitishwe.
Kura za wabunge waliotaka mjadala huo uendelee zilikuwa nyingi kutokana na
CCM kuwa na wabunge wengi. Lakini baada ya uamuzi huo, Mbowe alisimama kuomba
ufafanuzi wa kikanuni, akakataliwa.
Licha ya Ndugai kumdhalilisha Mbowe, hakufahamu alitaka kusema nini, hatua
iliyoibua hamaki kwa wapinzani.
Mbowe alitaka kuomba kiti kiwatake viongozi wa serikali, Mwanasheria Mkuu,
Jaji Fredrick Werema na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi waweke mezani ushahidi wa vielelezo vya taarifa
walizokuwa wamezitoa.
Kwa mujibu wa Mbowe, taarifa hizo hazikuwa na uthibitisho wa vielelezo, na
kwamba vile vile zilikuwa na upotoshwaji mwingi, lakini Ndugai hakumpa nafasi
hiyo, badala yake alimtaka aketi chini.
Kiongozi huyo, hakuketi bali alisisitiza kuwa ana hoja asikilizwe, jambo
lililomfanya Ndugai kuwaita askari ili wamtoe nje bila kujali kama wengine
hawapaswi kuingia ukumbini wakati Bunge linaendelea kwa mujibu wa kanuni.
Baada ya askari hao kuitwa na kuingia ndani, wabunge wa upinzani ukimwondoa
Augustino Mrema wa TLP (Vunjo), walimzunguka Mbowe wakipinga asitoke nje kwa
kuzingatia kuwa Ndugai alikuwa amekiuka kanuni.
|
No comments:
Post a Comment