Kushoto ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wa CCM, Mkoani
Mbeya, Fatuma Kasenga (aliyekumbwa na dhahama hiyo), akiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo wilayani Rungwe, Mwalimu Peter Gwandege Nkanje.
Wananchi wa Kata ya Kambasegela
wilayani Rungwe mkoani hapa, wamewafukuza viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM
wa kata hiyo walipotaka kufanya mkutano wa hadhara ili kuimarisha chama chao.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika
ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga, Katibu
wa jumuiya hiyo Kata ya Kambasegela, Frank Mwansasu, alisema wananchi
walimtimua yeye na msafara wake kwa madai kwamba waliahidiwa maji zaidi ya
miaka kumi sasa bila kupatiwa.
“Mwenyekiti, kero yangu kubwa ni
kwamba, mimi na wenzangu tulifukuzwa na wananchi tusifanye mkutano wa hadhara
wakati wa ziara yetu ya kata, wananchi wanasema waliahidiwa maji, lakini
hawajapelekewa mpaka hivi sasa,” alisema Mwansasu.
Akijibu kero hiyo, Mwenyekiti
Kasenga, alisema hayo ni matokeo ya baadhi ya viongozi kutowajibika vema katika
nafasi zao.
Alisema suala hilo limemsikitisha,
na kwamba yeye na msafara wake watalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Mbeya, Godfrey Zambi, ili kulipatia ufumbuzi.
Akiwa katika ziara hiyo, mwenyekiti
huyo alipokea kero nyingine kwa baadhi ya wananchi wa Kata ya Nkunga, ambao
walimwambia kuwa chama hicho kinachukiwa kwa udhaifu wa baadhi ya viongozi
wake.
Wananchi walisema kata hiyo ina
uhitaji wa umeme, na kwamba katika Kijiji cha Ibililo, kuna msigano wa
viongozi, jambo ambalo linasababisha kutopatikana kwa maendeleo ya kijiji.
“Jitokezeni kwenye marekebisho ya
daftari la kudumu la mpiga kura na ukifika wakati wa uchaguzi, wazee, vijana na
wanawake wanaofaa wapeni nafasi wagombee,” alisema Kasenga.
- Gordon Kalulunga
·
No comments:
Post a Comment