BAADA
ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kumshambulia Mbunge wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), ukimuita mpangaji katika jimbo hilo,
amewajibu akisema kuwa wanaota ndoto za mchana.
Mbilinyi
maarufu kama Sugu, alisema vijana hao hawazijui siasa za jimbo hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa jana, Sugu, alisema vijana hao
ndio wapangaji, na kwamba wasitarajie mteremko kwani yeyote atakayesimamishwa
katika jimbo hilo kupitia CHADEMA ataibuka mshindi kutokana na wananchi wa
Mbeya kuendelea kuwa na imani na chama hicho.
Alisema
jimbo hilo alilikuta kama nyumba mbovu, akaamua kuinunua na baadaye akaivunja
na kupandisha ghorofa, halafu aliyemuuzia anarudi na kudai nyumba ni ya kwake.
“Ndugu
zangu, Jimbo la Mbeya ni sawa na Mkinga ama Mpemba aliyeenda Kariakoo, amenunua
nyumba chakavu akaibomoa na kupandisha ghorofa zaidi ya tatu, halafu aliyeuza
nyumba hiyo anaibuka na kusema hao watu ni wapangaji, si atakuwa anachekesha?”
alihoji.
Aliongeza
kuwa CCM hawana chao katika jimbo hilo kwa sababu sasa CHADEMA wanawaza
kuchukua Halmashauri ya Jiji, na kwamba suala la ubunge haliwapi shida tena.
“Mikakati
yetu ni kuchuka kata zote, lakini ili kuleta changamoto katika baraza ni vema
tukawaachia kata kama nane ili kuleta changamoto katika Baraza la Madiwani,”
alisema.
Kwa
mujibu wa mbunge huyo, viongozi hao wa UVCCM wanafanya mikutano hiyo bila kuwa
na taarifa kamili za jimbo hilo, kwamba ndio maana wamekuwa wakikurupuka na
kutoa shutuma zisizo na ukweli wala utafiti wowote.
Alisema
kuwa katika Kata ya Igawilo kulikuwa na mpango wa kujenga bwawa la samaki,
lakini diwani wa kata hiyo kupitia CCM aliwashawishi viongozi wa serikali
kugomea mradi huo kwa madai kuwa hitaji lao ni madawati.
Sugu
alisema kuwa utafiti alioufanya alibaini mradi huo uligomewa na viongozi wa
serikali za mitaa, ambao walipata shinikizo kutoka kwa diwani.
“Unajua
watu wanaongea sana, ohoo aliahidi kuwa ataleta mradi wa samaki na mpaka sasa
hakuna kitu, wananchi wengi hawajui, utekelezaji ulishaanza, lakini kutokana na
ukiritimba wa baadhi ya wanasiasa pamoja na watumishi wa serikali
wameukwamisha.
“Pale
Uyole Nsalaga tulishachimba bwawa la samaki muda mrefu na nilishaongea na
Mkurugenzi wa Jiji tukabaini kuwa maji yanayohitajika katika bili yake ni kama
sh 200,000 kwa mwezi, lakini mpaka sasa hakuna kitu, wanazungusha tu bila kutoa
sababu za msingi,” alisema Sugu.
Katika
mikutano mingi ya CCM, wamekuwa wakijinadi kuwa jimbo hilo limepangishwa kwa
muda kwa CHADEMA, hivyo uchaguzi ujao watalirejesha bila ugumu wowote.
Wakiongozwa
na Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika
sherehe za kuwaapisha makamanda wa UVCCM kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi
Ruanda Nzovwe mwishoni mwa wiki, vijana hao wa CCM walisema kuwa Sugu ni
mpangaji katika jimbo hilo, hivyo ajiandae kuondoka katika uchaguzi ujao.
No comments:
Post a Comment