WARAKA MUHIMU
NATAKA SUGU ASHINDE UBUNGE MBEYA
Na Ezekiel KamwagaMiezi michache iliyopita niliiona picha ya msanii maarufu wa muziki nchini, Ambwene Yesayah (AY), akimchangia kiasi cha sh 100,000 Mwanahabari Violeth Mzindakaya, kumsaidia kuwania ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu.Wakati huo, taarifa kwamba msanii mwingine wa muziki, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Mr II naye alikuwa mbioni kuwania ubunge hazikuwa wazi.
Kwa hiyo nilielewa hatua hiyo ya AY. Wanahabari wamefanya kazina wasanii wa fani mbalimbali. Na pengine AY aliona Mzindakaya anaweza kuwa msaada kwao kwa vile amefanya nao kazi na anafahamu shida zao.
Hata hivyo, sasa katika kipindi ambacho Mbilinyi ametangaza kuwa atawania ubunge katika jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nafikiri wasanii wanapaswa kumuunga mkono, ili apate nafasi hiyo.
Duniani kote, hasahasa katika nchi zilizoendelea, makundi mbalimbali huhakikisha kuwa yana uwakilishi wao bungeni. Na hili pia,kwa kiasi fulani lipo hapa kwetu.Bunge la Tanzania lina wabunge wa viti maalumu wanaowakilisha makundi mbalimbali nchini, kuanzia vijana, walemavu, wakinamama na vyuo vya elimu ya juu.
Mbilinyi anakuja na sura mpya katika uwakilishi huu, yeye atawakilisha vijana wanaoishi kwa kutegemea muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva.Katika hali ya kawaida wasanii wa Tanzania wanahitaji mwakilishi wao ndani ya Bunge letu tukufu. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, muziki wa Bongo fleva umekuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya ajira hapa nchini.
Ajira kwa vijana imepunguza baadhi ya matatizo ambayo yangeikumba jamii ya watanzania iwapo vijana hawa wangeamua kufanya vitendo vingine.Nimesikia nyimbo nyingi za vijana hawa wakizungumzia namna muziki ulivyowaokoa kutoka kuwa majambazi, wabakaji na mateja. Nafikiri imefika wakati tunahitaji kuuheshimu muziki huu. Ndio maana nadhani ni muhimu kwa muziki huu kuwa na mtu wa kuusemea ndani ya chombo cha kutunga sheria na kuisimamia serikali.
Kilio cha wasanii kuhusu hakimiliki na unyanyasaji na unyonyaji unaofanywa kwa wanamuziki na wasanii Tanzania kitapata nguvu iwapo atakuwapo mtu wa kuwasemea bungeni. Binafsi kama ningeambiwa ni msanii gani wa Tanzania ningetamani apewe fursa ya kuingia Bungeni bila shaka ningemtaja Mr. II.
Nimesikia nyimbo zake kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita na amekuwa na ujumbe ambao unaeleza maisha halisi ya Mtanzania. Ameimba kuhusu namna umasikini unavyowaathiri Watanzania , ubaya wa uongozi bora na ameipigania fani ya muziki isionekane kuwa ya kihuni .
Ameitafuta haki ya kuwa mwakilishi wa wasanii wa Tanzania kutokana na rekodi ya kutetea haki zao kila wakati na kila mara.Nafahamu kwamba ndani ya bunge lililopita, alikuwapo John Komba ambaye sote tunafahamu ni msanii na alipaswa awe mtetezi wao Bungeni.
Tatizo langu na Komba ni kuwa yeye ni mtu wa kikazi tofauti na vijana wanaoishi kwa kutegemea Bngo fleva. Tangu miaka ya nyuma, yeye amekuwa kaitumika ndani ya chama na serikali. Hajawahi kusota katika namna ambayo wakina Mr. II walisoka katika siku za nyuma.
Hata kama albamu ya kundi lake la Tanzania One theatre (TOT) isipouza vizuri sokoni, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitahakikisha wafanyakazi wake wanalipwa mishahara yao kama kawaida.Kama albamu ya Diamond, Ngwair, Juma nature, Afande Sele, Lady JD, Profesor Jay, Ray C isipouza sokoni, hiyo inakuwa “imekula kwake”. Hawa hawana mjomba wa kuwalipa mshahara.
Ndio maana naamini wasanii wa Tanzania watafaidika sana na kuwakilishwa na mmoja wao kuliko kuwakilishwa na mtu mwingine.Huwezi kutarajia mbunge wa kundi la vijana akaenda kuwatetea wasanii kama ambavyo Mr. II atafanya. Si lazima mtu akiwa kijana basi ni lazima ajue kila tatizo linalowakumba wasanii.
Mbaya zaidi, wengi wabunge vijana wanaopata fursa katika siku za hivi karibuni, hupata nafasi hiyo ama kwa sababu ya kuwa “watoto wa wakubwa” au watu wanaotumwa na vigogo kwenda kuwawakilisha .Hawa hawana sababu ya kupaza sauti kuwatetea wasanii .hawa wanajua ni Baba ama Mama zao waliowafikisha hapo. Wawatetee au wasiwatetee wasanii, haitabadili chochote kwao.
Ningependa kuona wasanii wa Tanzania wakiungana kwa pamoja kumuunga mkono Joseph Mbilinyi kama kweli wanataka sauti zao zisikike kwa pamoja.Kama wanataka mtu azungumze kile wanachokitaka, kwa lugha yao na kwa namna yao, Mr II ndiye anayefaa.
Matukio ya karibuni zaidi yameonyesha kwamba Mr II haogopi mtu yeyote pale anapoona haki yake au ya wasanii wenzake zinaporwa na yeyote.Ninajua kwamba wapo watakaowaambia wasanii wasimuunge mkono Mr. II kwa vile anawania nafasi hiyo kupitia chama cha upinzani. Huu ni upuuzi mtupu.
Raisi mstaafu, Benjamin Mkapa, alipata kutamka katika siku za nyuma kwamba rangi ya paka haina maana yoyote isipokuwa uwezo wake wa kukamata panya wanaosumbua nyumbani.Kama paka anafanya kazi yake vyema, awe mweusi, mweupe au mwekundu haina maana yeyote. Wanachohitaji wasanii ni mtu wa kuwawakilisha Bungeni na si chama ca siasa.
Ningetamani kuona wasanii wa Tanzania wakifanya onyesho la pamoja katika jimbo la Mbeya Mjini kutangaza kumuunga mkono Joseph.Ningetaka kuona wasanii wa Tanzania wakihakikisha wako pamoja na Mr. II wakati wa kampeni kwa kupokezana ili kuhakikisha hakuna hata kipindi kimoja ambapo anabaki mwenyewe jukwaani.
Ninafahamu kwamba Mr. II hatajali sana kama ataachwa mwenyewe na wasanii wetu ambao watakuwa wakikimbizwa huku na huko na wanasiasa watakaotaka kutumia ushawishi wao katika kipindi hiki cha uchaguzi.Jambo la muhimu kwa msanii yeyote ili kushinda katika maisha haya ni kuwa na uwezo wa kusimama mwenyewe. Na Joseph amesimama mwenyewe katika miaka yake 15 ya fani hii.
Lakini kwa faida ya wasanii wa nchi yetu, kizazi cha sasa na kijacho, nadhani huu ni wakati muafaka wa kumuunga mkono mtu mmoja tuu …....... Joseph Mbilinyi A.k.a SUGU.
No comments:
Post a Comment