Mbunge wa Mbeya mjini,
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amelishutumu Jeshi la Polisi mkoani humo kuwa ndiyo
chanzo cha vurugu baada ya juzi kutumia mabomu ya machozi kuwazuia wafuasi wa
Chadema na waombolezaji kuubeba mikononi mwili wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa
wa Itiji, Ezekiel King kwa lengo la kutembea nao kwa miguu kutoka
Hospitali ya Rufaa Mbeya hadi nyumbani kwake Itiji kuuzika.
Baada ya mabomu hayo
kurushwa, viongozi na waombolezaji walilazimika kulibwaga chini jeneza la mwili
wa marehemu na kuanza kukimbia.
Marehemu alifariki dunia
katika hospitali hiyo, alikopelekwa kwa ajili ya matibabu baada ya kuugua
ghafla katika Gereza la Ruanda alikokuwa akitumikia kifungo cha miaka saba
baada ya kupatikana na kosa la kudhuru mwili wa mwanachama wa CCM .
Akizungumzia tukio hilo,
Sugu alisema kilichotokea juzi ni uthibitisho kwamba polisi ndiyo wamekuwa
chanzo cha vurugu.
“Sisi tulikuwa kwenye
msafara wakaja kutuzuia na kuninyooshea bunduki. Tukawaeleza tunakwenda kuzika,
wao wanasema tulitakiwa kuomba kibali cha kwenda kuzika,” alisema Sugu na
kuongeza: “Watu walikuwa wengi na magari ya kuwabeba kwenda kuzika hayakuwepo,
tuliamua kutembea sasa kibali cha nini,” alisema Sugu.
Sugu alisema polisi
wasipobadilika mara moja, wananchi watachukua hatua kuwaondoa katika nyumba
walizopanga uraiani ili wakaishi kituo kikuu cha polisi mkoani humo kwa vile
hawaijali jamii inayowazunguka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed
Msangi aliwataka Chadema kuacha kuwazushia polisi na kuongeza kuwa madai ya
Sugu hayana ukweli wowote.
- Mwandishi Wetu, Mwananchi
No comments:
Post a Comment