Mbilinyi, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alitoa majigambo hayo jana wakati akisoma maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Azimio la Serikali la Kuridhia Mkataba wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) la Kulinda Urithi wa Utamaduni Usioshikika wa mwaka 2003.
Azimio hilo liliwasilishwa jana bungeni na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi. Kabla ya kutoa maoni hayo, Mbilinyi alisema, “Kwa heshima kubwa niwashukuru wananchi wa Mbeya Mjini kuniwezesha kuweka historia ya kuwa msanii wa kwanza wa Bongo Flava kuchaguliwa kuwa Mbunge, Mheshimiwa Spika, mimi na wewe tumeingia katika historia kupitia Bunge hili la kumi, kwa mimi kuwa msanii wa kwanza wa Bongo Flava kuingia bungeni na wewe kuwa Spika wa kwanza mwanamke kuliongoza Bunge,” alisema Mbilinyi na kufanya wabunge kuangua kicheko.
Mbilinyi baada ya kueleza kuwa suala hilo ni la kihistoria na yeye anafarijika ameingia katika historia, alimpongeza Makinda na kuendelea kutoa maoni ya kambi ya upinzani yaliyounga mkono hoja hiyo na kueleza kuwa azimio linalenga kulinda hadhi ya Mtanzania.
Baada ya maoni ya Kambi hiyo ya Upinzani, baadhi ya Wabunge walipata fursa ya kuchangia azimio akiwemo msanii mwingine, Mbunge wa Viti Maalum, Vick Kamata (CCM) ambaye aliunga mkono hoja na kueleza kuwa mkataba huo ukiridhiwa utawawezesha wasanii kutambulika kimataifa na kazi zao kuweza kulindwa kwa kuwa suala la hatimiliki limezingatiwa kwa upana katika mkataba huo.
Naye Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama (CCM) alisema kilio cha wasanii wa nyimbo za asili zinazobeba utamaduni wa Kitanzania, kimefika mahali pake na kutaka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, kupigwe nyimbo za asili za makabila yetu badala ya nyimbo za kigeni zinazopigwa hivi sasa.
No comments:
Post a Comment