Jaji Mstaafu Lameck Mfalila
JAJI mstaafu wa Mahakama ya Rufaa nchini, Lameck Mfalila, amewataka Watanzania kuchagua mgombea aliyethubutu kusema; "atasomesha wanafunzi na kutoa huduma ya afya bure." Akitetea msimamo huo, Jaji Mfalila alisema:"Huyu ni shujaa, sio ghilba bali amethubutu kusema anaweza kufanya mabadiliko hayo, mchagueni."
Katika mkutano wa wanaharakati kuhusiana na Uchaguzi Mkuu jijini Dar es Salaam jana, Jaji Mfalila alitoa sifa kwa mgombea mmojawapo wa urais kutoka kambi ya upinzani ambaye ameweka wazi kwamba akiingia Ikulu, elimu na afya zitatolewa bure.
“Kuna mgombea mmoja kutoka kwenye vyama vya upinzani, naona anaitia changamoto serikali, yeye alithubutu kusema ikiwa atachaguliwa kuingia Ikulu, atasomesha wanafunzi na kutoa huduma ya afya bure, huyu ni shujaa, sio ghilba bali amethubutu kusema anaweza kufanya mabadiliko hayo, mchagueni,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Jaji Mfalila, ikiwa wananchi watafanya mabadiliko hayo wataweza kupata kiongozi bora atayesimamia mali asili za nchi yake vizuri.
Ingawa hakumtaja mgombea huyo, lakini wagombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa na wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba ndiyo ambao wamekuwa wakitoa ahadi hiyo ya kutoa elimu na afya bure kama wakishinda uchaguzi.
Kwa upande wa Dk Slaa, amekuwa akisema iwapo Chadema itapewa ridhaa ya kuongoza nchi, fedha zilizoporwa kifisadi zitarejeshwa na kuwa mwanzo wa kutoa elimu na afya bure kwa wananchi.
Ahadi yake hiyo ilimsababishia Dk Slaa kuingia katika mgogoro na Spika wa Bunge aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta, aliyepinga sera ya wapinzani ya kutoa elimu bure akisema kuwa haiwezekani.
Naye Prof Lipumba mara kadhaa amenukuliwa akisema kama akichaguliwa kuwa rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Serikali yake itaondoa gharama za elimu katika ngazi zote.
Lipumba alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akijinadi katika mikutano tofauti ya kampeni iliyofanyika mkoani Lindi na Mtwara.
Lipumba alisema CUF imeazimia kuweka suala la elimu ya bure katika vipaumbele vyake, kwa vile sekta hiyo ni mkombozi wa umaskini uliokithiri kwa wananchi wengi.
Katika mkutano huo wa jana, Jaji Mfalila alisema Tanzania ina kampuni kubwa ambazo zinafanya shughuli za kuzalisha madini yakiwamo ya dhahabu na almasi, jambo ambalo lingeweza kuingiza kiasi kikubwa cha fedha, lakini kutokana na ujanja uliopo makampuni hayo yanalipa kiasi kidogo cha kodi huku yakiwanufaisha wachache.
Jaji Mfalila ambaye alitumia zaidi ya saa moja kuitafakari serikali, ilipotoka, ilipo sasa na inapokwenda, alisema kuwa rasilimali zilizopo zinatumika kiujanja ujanja jambo ambalo limesababisha nchi kutegemea misaada kutoka kwa wahisani na nchi marafiki.
Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kufanya mabadiliko ya kumchagua kiongozi atakayeweza kuleta maendeleo kwenye taifa lake, hasa katika nafasi ya rais ambayo ndio injini ya maendeleo.
“Tanzania bila ya misaada inawezekana, tuna rasilimali za kutosha ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo. Wananchi wanapaswa kufanya mabadiliko ya kumchagua kiongozi anayeweza kuthubutu kuleta maendeleo hayo, chagueni upinzani kwa ajili ya maendeleo,” alisema Jaji Mfalila.
Jaji Mfalila alisema nchi nyingi duniani zilizopiga hatua kimaendeleo zilitumia rasilimali zake vizuri bila ya kuingiza ujanja ujanja.
Akizungumzia kilimo, Jaji Mfalila alisema kwamba inashangaza kilimo cha Tanzania mpaka sasa kinategemea mvua za misimu na pale ambapo mvua hizo hazinyeshi, viongozi wanaitana Ikulu kutafuta nchi ya kuomba msaada wa chakula wakati ardhi yenye rutuba ipo.
“Hii ni aibu ya kutosha kuona tunaomba msaada wa chakula wakati tuna ardhi bora kwa ajili ya shughuli za kilimo, lakini bado tunasubiri mvua ya miezi mitatu ambapo isiponyesha viongozi wanaitana Ikulu kwa ajili ya kutafuta nchi ya kuomba msaada wa chakula, kweli tunahitaji mabadiliko," alisema.
Akizungumzia enzi za uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, Jaji Mfalila alisema wanafunzi wa chuo kikuu waliweza kupatiwa mahitaji yote muhimu ili wasome kwa umakini zaidi, lakini siku hizi fedha za matibabu, chakula na kulipia gharama za ada zimekuwa tatizo kwao.
“Nasikia tu wanafunzi wamegoma kwa ajili ya kukosa fedha za ada, chakula na matibabu wakati enzi zetu tulikuwa tunakabidhiwa hundi ya malipo kabla ya kufika shuleni,”alisema.
Naye Profesa Chris Peter Maina, wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma ya Sheria Zanzibar, aliunga mkono kauli iliyotolewa na Jaji Mfalila akisisitiza kuwa elimu yaweza kutolewa bure.
“Nimesoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi nilipopata shahada yangu ya uzamili. Sharti kuu lililokuwapo ni kwamba nilihitajika kujaza fomu kuazimia kuwa nitalitumikia taifa langu baada ya kuhitimu masomo yangu,” alisema Profesa huyo.Aliongeza: “Kama nisingepata elimu ya bure, leo hii ningelikuwa nachunga ng'ombe kijijini kwetu.”
Profesa Maina alisema tatizo kubwa linaloikabili Tanzania ni kwamba viongozi wamevigeuza vipaumbele juu chini kwa kuwapa wakaguzi wa elimu wanaotumia magari ya Sh 150milioni yaliyo na viyoyozi kazi ya kukagua madarasa yasiyo na madawati na yenye wanafunzi wanaoketi chini.
“Sielewi ni kwanini mpaka leo miaka 50 baada ya uhuru wanafunzi wa Tanzania bado wanaketi chini kwenye madarasa yao?” alishangaa Profesa huyo wa sheria.